November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Minyoo inaweza kusababisha tatizo la akili

Na Aveline Kitomary,TimesMajira online,Dar es Salaam.

MINYOO ni aina ya vimelea vinavyoweza kuishi ndani ya kiumbe hai ili kujipatia mahitaji ya  chakula, hewa na kila wanachohitaji ndani ya viumbe wanamoishi.

Vimelea hivyo wanaotambulika kwa  jina la parasitic worm wakiwa ndani ya  mwili wa kiumbe hai kusababisha madhara makubwa ya afya .

Huzaliana kwa kutaga mayai wakiwa ndani au nje ya mwili wa mwanadamu na huwa na uwezo wa kudumu miezi kadhaa bila ya kufa na kuvumilia hali iliyopo.

“Ndani ya mwili minyoo hutumia chakula alichokula binadamu,wapo minyoo wanaishi kwenye utumbo mdogo,” anaeleza Afisa Mtafiti wa Lishe Kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Dk.Analace Kamala.

Utumbo mdogo ndiyo sehemu ambayo chakula kinameng’enywa na kuupa mwili virutubishi.

Lakini minyoo hawa wakati mwingine wanakula chakula alichokula mtu hata kabla ya kumeng’enywa,hula tishu nyingine, kwenye ngozi na viungo vingine vya mwili.

Wapo minyoo hunyonya damu huku wengine wakiishi kwenye mfumo wa damu ama maeneo mengine na kuanza kunyonya damu huku wakila viungo vya mwili .

“Wanaoishi kwenye ini ama maeneo ya nyongo,minyoo hawa wanakula ini, na kulisababishia vidonda, pia ini linaweza kuvimba hatimaye kuleta madhara makubwa,

“Maambukizi hutokana na udongo uliochafuliwa na kinyesi cha binadamu  ambacho kina mayai ya minyoo ambapo minyoo  wanaweza kuishi kwenye kinyesi vyema na kwa muda mrefu zaidi kuliko maeneo mengine,kama  mtu mwenye minyoo akitapakaza kinyesi chenye minyoo husambaza wadudu hao”anasema Dk.Analace.

HUSABABISHA TATIZO LA AKILI

Wakati mwingine ni vigumu kufahamu kama una minyoo, kwani minyoo wanaweza kukaa ndani ya mwili kwa muda mrefu bila kuonesha dalili yeyote.

Uwepo wa minyoo katika mwili huweza kusababisha matatizo ya akili kutokana na kuathiri mfumo wa fahamu hivyo kusababisha mtu kuwa na tatizo la akili.

“ Kila mtu yupo katika hatari ya kuathiriwa na minyoo lakini walio katika hatari zaidi ni watoto ambao hawajaanza shule kwa sababu wale watoto  mahitaji yao ya lishe ni makubwa sana na wanashambuliwa na magonjwa mara kwa mara  na pia wanawake walio katika umri wa uzazi nao wapo katika hatari”anasema.

Anasema minyoo hasa wanaosambaa kupitia udongo wapo nchi nzima ndio maana dawa za kutibu minyoo hutolewa kila mkoa huku baadhi ya mikoa akiitaja kuwa  na aina zaidi ya moja ya minyoo.

Dk.Analace anasema “Dalili za minyoo hutofautiana  kulingana na aina za minyoo, dalili kuu kama unasumbuliwa na wadudu hawa ni kichefuchefu,kukosa hamu ya kula,maumivu ya tumbo, uchovu wa viungo,kuona utelezi mwingi kama kamasi kwenye kinyesi,minyoo kwenye kinyesi,kuona damu kwenye kinyesi na tumbo kujaa”

Anasema, minyoo huwa na uwezo wa kusababisha upungufu wa damu mwilini kutokana na minyoo hao kufyonza damu na pia kusababisha mwili kukosa virutubishi kutoka kwenye chakula, kupungua uzito na kukonda,ukuaji hafifu kwa mtoto,na kupata matatizo yanayohusiana na ini na nyongo.

MINYOO INATIBIKA

Dawa za kutibu maambukizi ya minyoo hutolewa mara mbili kwa mwaka kupitia kampeni ya Mwezi wa Afya na Lishe ya Watoto inayotekelezwa Juni na  Desemba

Watoto wenye umri wa miezi 12 – 59 wapewe dawa za kutibu maambukizi ya minyoo kila baada ya miezi 6.

 Mkakati wa Mwezi wa Afya na Lishe kwa Mtoto, ni mojawapo ya mbinu ya kuwafikia watoto wengi na huduma ya matibabu ya maambukizi ya minyoo na kudhibiti tatizo la upungufu wa viinilishe na  udumavu.

Afisa  Lishe Mtafiti Mwandamizi TFNC  Francis Modaha  anasema, huduma za mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto (CHNM) huwalenga watoto wote katika  halmashauri zote nchini .

“Huduma hizi ni mojawapo ya mikakati ya kitaifa kwa ajili ya kuimarisha na kudumisha Afya na Uhai wa motto, huduma hizi za afya na lishe huwafikia watoto wengi kwa gharama nafuu lengo kuu kutoa huduma  jumuishi za kinga kwa gharama nafuu kuimarisha afya na uhai wa motto.

Na huduma za kawaida za afya ya uzazi na mtoto zitolewazo katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Modaha anataja huduma jumuishi za kinga zitolewazo kuwa ni vitamini A,dawa ya kutibu maambukizi ya minyoo na  tathmini ya hali ya lishe lengo likiwa ni kuongeza na kudumisha kiwango cha watoto wanaofikiwa kwa zaidi ya asilimia 90 mara mbili kwa mwaka kwa huduma za vitamini A  kwa watoto wote wenye umri wa miezi 6 hadi 59,kutibu  maambukizi ya minyoo kwa watoto wote wenye umri wa miezi 12 hadi 59,tathmini ya hali ya lishe kwa watoto  wote wenye umri wa miezi 6 hadi 59 na kuwatibu watoto wote wanaogundulika na utapiamlo.

“Walengwa, mahali na wakati wa huduma za Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto  ni watoto wote wenye umri wa miezi 6 hadi  59 katika Halmashauri zote nchini huduma hizi hutolewa katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya kote nchini “anasema.

Modaha anasema, mojawapo ya huduma zinazotolewa katika mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto ni utoaji wa dawa za kutibu maambukizi ya minyoo,  matibabu ya maambukizi ya minyoo ni mojawapo kati ya mikakati ya kukabiliana na tatizo la upungufu wa viinilishe na udumavu kwa watoto.

UNAWEZA KUJIKINGA

Dk.Analace anasema ili kujikinga na minyoo ni vyema matumizi ya vyoo kuzingatiwa ili kuboresha usafi wa mazingira,pia kunawa mikono kwa maji safi na sabuni,kutunza kucha zikiwa fupi ili zisihifadhi uchafu ndani.

Njia zingine ni kuchemsha nyama, samaki vizuri kabla ya kula na kutumia maji safi na salama kuandaa chakula au kunywa.

“Ili kujikinga watoto wasicheze au kuogelea kwenye maji yenye maambukizi,uvaaji wa viatu uzingatiwe  na kufukia maeneo yanayozalisha kichocho (mfano, mabwawa) kama hayahitajiki.

watoto wakipewa dawa ya minyoo

NI MUHIMU KUPIMAJI WA LISHE

Afisa Lishe Mwandamizi  TFNC  Wessy Meghjie anasema uchunguzi wa hali ya lishe ni muhimu kufanyika wakati unapotokea mwanya wa kukutana na watoto .

“Hii itasaidia kubaini/kuwagundua mapema watoto wenye matatizo la kilishe au utapiamlo kabla tatizo halijawa kubwa na kuwapatia matibabu stahiki, upimaji wa hali ya lishe hujumuishwa na zoezi zima la Mwezi wa Afya na lishe ya mtoto ili kuweza kuwafikia watoto wengi zaidi takribani milioni 8.5.

Watoto wenye utapiamlo wa kadiri bila matatizo ya kiafya watapewa rufaa kwaajili ya kutibiwa na kurudi nyumbani.Na wale wenye utapiamlo mkali na wa kadiri unaoambatana na matatizo ya kiafya watapewa rufaa ya usimamizi/matibabu unaotolewa kwa wagonjwa wanaolazwa”anasema

Wessy anasema,uvimbe unaobonyea ni dalili ya utapiamlo mkali kama utakuwepo katika miguu yote miwili.

Jinsi ya kuchunguza uvimbe unaobonyea,bonyeza miguu kwa kutumia vidole gumba kwa muda wa sekunde 3 kisha ondoa vidole vyako kama ngozi ya miguu yote miwili itabaki imebonyea hii itaonyesha kuwa mlengwa ana uvimbe unaobonyea, angalia iwapo mlengwa ana uvimbe unaobonyea sehemu za uso na mikononi.

MWISHOO..