November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa Chama cha mchezo wa Kabaddi Tanzania (TKSA), Abdallah Nyoni

Algeria nao wathibitisha kushiriki Kabaddi Afrika

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

NCHI ya Algeria imethibitisha kuungana na nchi nyingine  sita ikiwemo wenyeji Tanzania kushiriki mashindano ya mchezo wa Kabaddi ya Afrika ambayo yataanza kutimua vumbi rasmi kuanzia Juni 29 hadi Julai 5, 2021 jijini Dar es Salaam.

Awali mashindano hayo yalitakiwa kufanyika Desemba mwaka jana lakini yakasogezwa mbele hadi Februari, kisha Aprili ambapo pia yalibedilishwa tena hadi Juni baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Shirikisho la Kabaddi Afrika kilichofanyika Machi, 2021 kupitia Zoom ambacho walikubaliana kubadili tarehe kutokana na masuala ya janga la Corona kuendelea kuzikabili baadhi ya wanachama wake ambao watashiriki katika mashindano hayo.

Katika mashindano hayo ya Afrika nchi zote zitawakilishwa na timu za wanawake na wanaume na hadi sasa nchi zilizothibitisha kushiriki ni Kenya, Cameroon, Misri, Zimbambwe, Mauritania pamoja na Algeria ambao bado hawajataja idadi ya timu zitakazokuj huku Nigeria na Tunisia zenyewe zitatoa wawakilishi wao kuja kushuhudia mashindano hayo kwakuwa timu zao hazitashiriki.

Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo wa Kabaddi Tanzania (TKSA), Abdallah Nyoni ameuambia Mtandao huu kuwa, mbali na Algeria kuthibitisha ushiriki mashindano hayo lakini pia Kenya itaongeza timu ya Circle Kabaddi ambayo itachuana na timu ya Magereza kutokana hapa nchini.

Licha ya kuwa Ciecle Kabaddi itachezwa katika mashindano hayo lakini itakuwa kama sehemu ya onyesho kwani haitakuwa sehemu ya mashindano hayo.

Akitolea ufafanuzi hali ya kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Nyoni amesema, kwa sasa wachezaji wa kikosi cha timu za Tanzania wapo vizuri na wanaendelea vizuri na mazoezi kwani wachezahji wao wamejipanga kufanya vizuri na kuiwakilisha vizuri nchi katika mashindano hayo yatakayofanyika katika katuka uwanja wa ndani wa Taifa.

“Tayari timu kutoka nchi tano zimeshathibitisha kushiriki mashindano haya, na bado muda wa kuthibitisha bado upo hivyo tunaamini tutapata nchi nyingine ambazo zitathibitisha kushiriki mashindano haya ili kufanya ushindani kuwa mkubwa,“ amesema Nyoni.

Kwa sasa wanaendelea na shughuli zingine zilizopangwa kama ikiwemo kusaka udhamini, kutafuta mshirika wa kwa upande wa vyombo vya habari, maandalizi ya timu ya kitaifa, uuzaji na uendelezaji wa michezo ya Kabaddi.

Amesema, TKSA wamekuwa wakipata msaada mkubwa kutoka kwa washirika wake ambao ni Ofisi ya Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Michezo la Tanzania, Kamishna Mkuu wa India nchini Tanzania na Patroni wao ambaye amewapa msaada mkubwa hata katika kuiweka kambini timu ya Taifa.

“Ni matumaini yangu wataendelea kutuunga mkono katika maandalizi ya mashindano haya, lakini pia bado tunawakaribisha wadau wengine kutoa michango na ufadhili, tunahitaji udhamini zaidi kwa maandalizi ya timu ya Taifa haswa katika mechi za majaribio, kambi ya mazoezi. Mbali na hayo tunahitaji kununua vitu vyote muhimu ikiwa ni pamoja na jezi,” amesema Nyoni.