November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Password’ muhimu kwenye simu yako

Na Penina Malundo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

MKUU wa Kitengo cha Usimamizi na Utekelezaji wa Sheria wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania( TCRA), Dkt. Philip Filikunjombe amesema umuhimu kila mtu kuhakikisha anaweka nywila ‘Password’ kwenye simu yake.

Pia amewakaribisha Watanzania, kutoa maoni yao juu ya maboresho ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020, ili kanuni hizo ziwe rafiki katika matumizi.

Akizungumza hayo leo mkoani Morogoro wakati wa semina kwa Waandishi wa Habari Mtandaoni (Online Media Journalists, Bloggers and Editors) ili kuwajengea uwezo kuhusu Sheria mbalimbali zinazohusu Tasnia ya Habari iliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Amesema uwekaji wa password kwenye simu unasaidia kwa kiasi kikubwa mtu kutotumia simu yake bila idhini ya muhusika.

Amesema ni vema mtumiaji wa kifaa cha mawasiliano kuweka Password kwenye simu yake ili kulinda taarifa zake ikiwa ni pamoja na kuepuka watu wengine kutumia vibaya mtandao.

“Weka password kwenye simu yako na usimpe mtu mwingine namba yako ya siri hata kama ni mme au mke wako pia si vema kumpa mtoto simu ,”amesema na kuongeza

“Usimpe simu yako mtoto kwa sababu kuna mambo mengine hayapaswi kuonwa na watoto kwa umri wao”, amesema Dkt. Philikunjombe.

Akiongelea kuhusu Kanuni amesema lengo la mapitio ya kanuni hizo ni kuondoa kanuni ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele na wadau mbalimbali hususani za kihabari, kuwa zinakwaza upashanaji habari.

“Kama kuna kifungu fulani kina shida, toa maoni yako, usijiangalie wewe unapotoa maoni, uangalie namna gani kanuni iboreshwe na wafikilie wengine kwa kundi kubwa ili kuona kanuni ziboreshweje. Tunataka kuweka mambo mazuri zaidi,” amesema na kuongeza

“Kila nchi duniani, imekuwa ikitumia njia mbalimbali katika kuweka kanuni za matumizi ya maudhui mtandaoni na Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi hizo,”amesema