Na Mwandishi Wetu, TimesMajira online, Dar es Salaam
KATIBU wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Nevile Meena amechukua fomu leo ya kuwania nafasi ya uenyekiti wa jukwaa hilo.
Meena amejitokeza katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya mwenyeki wa jukwaa hilo ili kuongoza nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minne. Amechukua fomu na kisha kujaza na kumkabidhi Mratibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Prisca Kabendera leo katika ofisi za TEF Jijini Dar es Salaam.
Meena ameeleza dhamira yake ya kuwania nafasi hiyo ya kuliongoza jukwaa ili kufikia malengo yake katika kipindi kijacho cha uongozi.
“TEF ndio chombo kikubwa kabisa nchini kinachounganisha wahariri na wadau kutoka katika vyomba mbalimbali vya habari nchini na tasnia nzima ya habari nchini hivyo nimechukua fomu baada ya kujitathimini na kuona kuwa natosha sasa kuwa mwenyekiti wa TEF baada ya kuwa na uzoefu wa kipindi cha miaka 10.
“Naamini tutakuwa TEF moja, nguvu moja na yenye nia moja na kuwa chombo chenye kuthamini mchango unaotolewa na waandishi wa habari nchini ,” amesema.
Meena amekuwa katibu wa TEF kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 amesema endapo atachaguliwa kuwa mwenyekiti TEF atahakikisha kuwa anaweka mifumo ambayo italeta manufaa kwa kila mhariri ambaye atakuwa ni mwanachama wa jukwaa hilo.
“Kutakuwa na mifumo ambayo kila mhariri atanufaika nayo naamini kama nitachaguliwa mengi nitayafanya kutokana na ushirikiano nitakaopewa na wahariri na pia kuhakikisha kuwa wahariri wanajiunga kwani mpaka kuna wanachama 110 na bado kuna wahariri wengi kwenye vyumba vya habari wenye sifa.
“Waswahili wanasema kuwa ‘Umoja ni nguvu,utengano ni dhaifu hivyo kutokana na umoja nitakaokuwa nao na wana-TEF naamini kuwa utaleta manufaa na nimekuwa katibu kwa kipindi kirefu hivyo na mengi nayajua na mengine yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuleta manufaa kwa waaandishi wa habari nchini,” amesema.
Amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TEF atahakikisha kuwa TEF inakuwa na nguvu kama zilivyo taasisi nyingine zinazotoa matamko ili kuhakikisha kuwa haki za waandishi zinapatikana.
TEF inatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu Mei mwaka huu ambapo itapata safu mpya ya uongozi ambayo itaongoza kwa kipindi cha miaka 4.
Mratibu wa TEF, Prisca amesema mpaka sasa wajumbe wengi wameshachukua fomu ili kuwania nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti pamoja na nafasi za wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
“Mwamko ni mkubwa, mijadala pia ni mingi na wajumbe wamejitokeza na kuchukua fomu kuonesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali za TEF hivyo nitatoa orodha ya wanachama waliochukua fomu na kuwania nafasi mbalimbali za TEF,” amesema Prisca.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
HAYA HAPA MATOKEO YOTE FORM II NA DARASA LA IV
Ufaulu waongezeka matokeo ya Darasa la Nne na Kidato cha Pili