Na Penina Malundo, TiimesMajira,Online, Dar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemlilia aliyekuwa mmoja wa wadau wakubwa wa vyombo vya habari nchini na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Montage, Teddy Mapunda aliyefariki dunia Mei 4,2021 baada ya kuugua ghafla.
Teddy aliugua wakati akipata futari na wenzake katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam na kukimbizwa hospitali ya Aga Khan, alipokutwa na mauti.
Chama hicho kimesema Marehemu Teddy aliweza kugusa maisha ya watu wengi kutoka kada mbalimbali, hivyo taifa limempoteza Mtanzania makini aliyejawa hisia za uzalendo na utaifa.
Akizungumza na vyombo vya habari kabla ya mazishi kufanyika nyumbani kwa marehemu Mbezi Beach ,Katibu wa Itikadi na Uenezi (NEC),Shaka Hamdu Shaka kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amemtaja Teddy kuwa alikuwa Mtanzania aliyependa habari muhimu za kitaifa ziwafike wananchi wanaoishi vijijini na mijini kwa haraka na usahihi .
Amesema Chama chao kitamkumbuka kwa ucheshi, huruma,upendo wake ,akiwa si mwenye majivuno , asiyedharau wenzake lakini pia hakupenda kujikweza.
Shaka amesema Marehemu Teddy amekuwa na kiu na mbinu za uwezeshaji wa kutosha ili habari ziweze kuwafika wananchi hususani wanaoishi mijini na vijijini na kuitangaza nchi yake hasa alipokuwa akifanyakazi katika Mbuga ya wanyama ya Taifa Serengeti.
“Hayati Teddy sifa yake kubwa ilikuwa ni unyenyekevu, ucheshi na mwenye moyo wa huruma ,alikuwa ni Mtanzania mzalendo, mtaifa na mchapakazi aliyependa kuona umoja wa kitaifa ukidumu nchini” Amesema Shaka
Amesema atakumbukwa kwa tabia yake na mwenendo bora na udilifu kwani hakuwa mtu mbabaishaji na asiyevunja wala kutotimiza miadi mnapowekeana ahadi kwani aliheshimu wakati.
“Tuige maisha aliyoishi mwenzetu hapa duniani kwani hakuwa mtu wa majivuno,hakuwa akivunja miadi pia hakupendelea wala kuwa na roho ya korosho. Mikono yake haikuwa kama ile ya birika.Badala yake alipenda kuwasaidia wenzake kila alipoweza na kuitazama jamii”Ameeleza .
Aidha Shaka amesema ni watu wachache mno duniani pale wanaopata nafasi hujikuta wakizitumia vibaya kuwakomoa wenzao , kuwanyanyasa na kuwapuuza wengine jambo ambalo katika maisha ya Teddy ilikuwa ni kinyume na hivyo.
Katibu huyo wa NEC itikadi na uenezi aliwahimiza watu wengine kutambua kuwa wanadamu katika dunia wana safari fupi hivyo kila mmoja ajijue iko siku ataondoka duniani na kurudi kwenye vumbi.
Shaka amesema chama cha Mapinduzi kinatuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na kumuomba Mungu awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwao cha msiba na maombolezo ili mungu amuweke mahali pema peponi . Teddy amezikwa leo katika Makaburi ya Kinondoni jijini humo.
More Stories
TARURA Kilimanjaro yatimiza ahadi ya Rais Samia
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime