November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NSSF yajipanga ‘kufyeka’ kero za wanachama

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Morogoro

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amemuhakikishia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, kuwa katika Mpango na Bajeti ya Mfuko ya mwaka ujao (2021/2022), wamejikita zaidi katika vipaumbele saba.

Kwa mujibu wa Mshomba vipaumbele hivyo saba vinaenda kuondoa kero mbalimbali hasa za wanachama.

Mshomba ameyasema hayo mwishoni mwa wiki, wakati wa uzinduzi wa Baraza jipya la 47 la Wafanyakazi wa NSSF lililofanyika mkoani Morogoro.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba akizungumza katika kikao cha 47 cha Baraza jipya la Wafanyakazi wa NSSF mkoani Morogoro. Mkutano huo ulifanyika mwishoni mwa wiki.

Kwa mujibu wa Mshomba, vipaumbele hivyo ni kama ifuatavyo;

Kuandikisha wanachama

Ametaja kipaumbele cha kwanza, ni kuhakikisha wanaandikisha wanachama katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi

Kuboresha huduma

Kipaumbele cha pili, Mshomba amesema ni uboreshaji wa huduma, kwani kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wanachama, hivyo wameelekeza nguvu katika kulitekeleza hilo.

“Tutahakikisha mifumo yetu (NSSF), iko vizuri na inakidhi matarajio yetu, katika hili tutatumia Tehama kuhahikikisha kazi zetu zinakwenda vizuri na huduma kwa wateja zinatolewa,” amesema.

Mafunzo kwa wafanyakazi

Mshomba amesema kipaumbele cha tatu, ni mafunzo kwa wafanyakazi ili waweze kuelewa taratibu za Mfuko.

Mafunzo ya watoa huduma kwa wanachama

Kipaumbele cha nne, amesema ni mafunzo kwa wafanyakazi watoa huduma kwa wanachama ili waweze kuvaa viatu vya wanachama kwa kuzingatia maadili ya Mfuko.Kujenga timu moja

Amesema kwamba kipaumbele cha tano, ni kujenga timu mmoja kwani bila ya kuwa na timu moja katika Mfuko mkubwa kama huo wanaweza wasifikie malengo, hivyo watawafanya wafanyakazi kuwa sehemu ya mfuko huo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (wanne kulia), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Baraza jipya la 47 la Wafanyakazi la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), mara baada ya kulizindua Baraza hilo mkoani Morogoro, mwishoni mwa wiki.

Kuwekeza mazingira bora ya kazi

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kipaumbele cha sita, wataweka mazingira bora ya kazi kwani ni jambo muhimu na kwamba amemuomba Waziri Mhagama kuwaunga mkono.

Usimamizi madhubuti wa menejimenti na Bodi

Kipaumbele cha saba, amesema ni usimamizi madhubuti hasa kwa Menejimenti na Bodi kwamba katika kutoa huduma bora lazima usimamizi uwe madhubuti ili waweze kufanikiwa katika malengo yao.

Kauli ya Waziri Mhagama

Akizindua Baraza hilo jipya la 47 la wafanyakazi wa NSSF, Waziri Mhagama, ameiiagiza Menejinti ya NSSF kuweka mifumo sahihi itakayoondoa changamoto za wanachama na wadau.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akizungumza wakati akifungua Baraza jipya la 47 la Wafanyakazi wa NSSF mkoani Morogoro.

“Nawaomba mkatathimini mifumo iliyopo na ikiwezekana mtengeneze mifumo ambayo itamuwezesha mwanachama kulipwa mafao yake bila kwenda kupiga magoti kwa wafanyakazi wa NSSF,” alisema.

Waziri huyo amewataka watumishi kuendeleza kasi ya kukusanya michango ya wanachama kwenye maeneo yote ya ajira ili inapotokea mfanyakazi amepata janga lolote, Mfuko uweze kumlipa kwa wakati na bila ya usumbufu.

Kauli ya TUICO

Naye, Mwakilishi kutoka Chama Cha Wafanyakazi wa Viwandani, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) na Mkuu wa Sekta za Taasisi za Fedha, Willy Kibona, amesema maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mhagama yamekuwa ni funzo kwa Baraza hilo jipya pamoja na watumishi wote wa Mfuko na kuahidi kuyatekeleza na kuyazingatia kama alivyoelekeza.

Ameishukuru Menejimenti na wafanyakazi wote kwa ushirikiano walionao kwamba wanaendelea kuzingatia kanuni na taratibu za sheria ambazo Wizara inazisimamia.

Wajumbe wa baraza la 47 la Wafanyakazi la Nssf wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati akifungua Baraza hilo mjini Morogoro, mwishoni mwa wiki.

“Tunasema asante sana wa kutujengea misingi imara ya kuanza tena awamu ya miaka mitatu ijayo ya Baraza hili hususani katika kutuasa yale yote ambayo tunatakiwa kuyatekeleza kwa mujibu wa sheria ya NSSF,” amesema.