Judith Ferdinand,timesmajira,Online,Mwanza
MBUNGE wa Jimbo la Ilemela,Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula amewaunga mkono waumini wa dini ya kiislamu katika kutimiza ibada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuwapatia vyakula kwa ajili ya futari.
Dkt.Angeline ametoa futari hiyo kwa kundi la yatima,wajane,wazee na watu wenye mahitaji maalum katika misikiti mbalimbali inayopatikana katika Kata zote 19 zilizopo jimboni humo wilayani Ilemela mkoani Mwanza zinazounda Jimbo hilo.
Akizungumza wakati akikabidhi futari hiyo kwa niaba ya Mbunge huyo,Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Kazungu Safari, amesema ili kuunga mkono juhudi za waumini hao katika kutimiza nguzo muhimu ya dini yao ya kati ya zile tano zilizoamrishwa na Mwenyezi Mungu Mbunge huyo ameona vyema kuungana nao kwa kuwapatia futari hiyo.
Kazungu amesema,jumla ya watu 400 kutoka katika makundi ya yatima, wajane,wazee na wenyewe uhitaji maalumu ndio wamewapatia futari hiyo.
Amesema,kabla ya futari hiyo pia Mbunge huyo alitoa Masaafu(Qur’an) 240 kwa ajili ya madrasa zilizopo katika jimbo la Ilemela.
“Mbunge anaamini kunapokuwa na waamini,watu wanao amini,tunakuwa na jamii iliyostarabika lakini ni jamii inayoendelea,kwahiyo yeye mwenyewe pasipo kujali itikadi za dini ameendelea kuwa na nyinyi katika nyakati nyingi hata leo ametutuma kuja kwenu na sadaka hii ili kuwashika mkono nyinyi katika mfungo huu mtukufu wa Ramadhani ambao ni muhimu kwa Jimbo,taifa na dunia nzima ya kujiweka karibu na Mungu,” amesema Kazungu.
Kwa upande wao waumini hao waliopata futari hiyo akiwemo Hamisa Salehe,amemshukuru Mbunge huyo kwa kuwawezesha futari katika mwezi huo wa Ramadhani ambayo ni sadaka,hivyo aliwaomba wengi ambao siyo waumini wa kiislamu wawe na moyo wa kuweza kuwatolea sadaka kama alivyofanya Dkt.Angeline.
Naye Aisha Twaha amesema,Jimbo la Ilemela limepata neema kwani suala la Dkt. Angeline kuwapa sadaka kama hizo siyo jambo la mara moja Ila limekuwa la mara kwa mara hasa ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani amekuwa akiwaita yatima,wajane,wazee na wasiojiweza anawapatia sadaka.
Hivyo alitoa wito kwa viongozi na watu wa maeneo mengine wa dini tofauti na wao waislamu wasifanye ubaguzi Mungu ni mmoja hivyo wawasaidie kama alivyo Dkt.Angeline ambaye amekuwa hana ubaguzi.
More Stories
Gavu aanika miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita Geita
RC Makongoro: Samia aungwe mkono nishati safi ya kupikia
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza