Na. Catherine Sungura, WAMJW, Shinyanga
MKOA wa Shinyanga umepokea fedha kiasi cha shilingi milioni 167.4 pamoja na kinga tiba kwa ajili ya zoezi la ugawaji wa kinga tiba hizo kwa halmashauri zote za mkoa huo kwa watoto wenye umri wa kwenda shule.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack wakati wa kufungua kikao kazi cha uraghibishaji na uhamasishaji wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kilichoandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele.
Telack amesema mkoa wake umejipanga vizuri kwa ajili ya kutekeleza zoezi hilo ambalo linatarajia kuanza mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu kwa wanafunzi wote wenye umri wa miaka mitano hadi kumi na nne.
Aidha, Telack amewataka Wakurugenzi wa halmashauri zote za Shinyanga kuwezesha zoezi la ugawaji wa kinga tiba za Kichocho na Minyoo ya tumbo ili kudhibiti magonjwa hayo na kujenga mazingira mazuri ya kuhakikisha watoto wote wanafikiwa.
“Magonjwa haya yameathiri jamii yetu na kuleta ulemavu hali ambayo imeleta usumbuvu kwa wananchi na watoto kutokuweza kuhudhuria vizuri masomo yao vizuri na kupunguza rasiliamali chache tulizonazo”.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa huyo amewahakikishia wananchi kwamba kinga tiba hizo ni salama na zimethibitishwa na Shrika la Afya Duniani(WHO) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) hivyo kuwataka wale wenye imani potofu kuondoa dhana hiyo.
Vile vile Telack amewataka wataalam wa afya na elimu kuwaeleimisha wananchi kwenye maeneo yao kwa kuwapa ujumbe sahihi ili itakapofika zoezi hilo kuweza kutokomeza tatizo hili katika mkoa wao.
Naye Afisa Mradi kutoka Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele, wizara ya afya Isaac Njau amesema zipo athari nyingi za muda mfupi na mrefu zitokanazo na kichocho kwa wanaume, wanawake na watoto ikiwemo Udumavu, utapiamlo, kuvimba Ini, kuharibika kwa mimba, Kanda ya kibovu Cha miojo pamoja na upungufu wa Damu mwilini.
Njau alitaja Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele ni pamoja na Usubi,Trackoma,Kichocho,Minyoo ya Tumbo,Matende na Mabusha(Ngirimaji).
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja