Na Edward Kondela,Timesmajira Online. Dodoma
BALOZI wa Vietnam nchini, Nguyen Nam Tien amesema atawasilisha serikalini vigezo vinavyopaswa kufuatwa na wafanyabishara wa Tanzania, ili waweze kusafirisha mifugo na nyama kwenda Vietnam kutokana na nchi hiyo kuwa na uhitaji mkubwa wa nyama.
Hayo yamesemwa juzi na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki jijini hapaa mara baada ya kuwa na mazungumzo mafupi na balozi huyo aliyefika ofisini kwake, ili kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam na kupeana uzoefu katika sekta za mifugo na uvuvi.
Ndaki amesema Balozi Tien, amesema nchi yake ina uhitaji mkubwa wa nyama kwa kuwa wana ng’ombe wasiozidi milioni sita, hivyo kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa hiyo endapo watakidhi vigezo vya kusafirisha mifugo na nyama nchini humo.
“Tunaweza kutumia fursa hii kusafirsha ng’ombe, au nyama na kwamba wataleta orodha ya vitu vinavyohitajika, ili kama nchi tuweze kupeleka ng’ombe au nyama,” amesema.
Waziri Ndaki amewaomba wawekezaji kutoka Vietnam, kuwekeza hapa nchini katika viwanda vya maziwa kwa kuwa maziwa yaliyopo bado ni mengi kulinganisha na viwanda vilivyopo, pamoja na kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata ngozi za mifugo kwa kuwa kiasi kikubwa cha ngozi kimekuwa kikiharibika.
Kuhusu Sekta ya Uvuvi, Waziri Ndaki amesema amemuomba Balozi Tien, kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo ili kuja kuwekeza katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na mabwawa kwa kuwa nchi hiyo, inafanya vizuri kwenye sekta hiyo.
Amefafanua kuwa lengo la Serikali ya Tanzania ni kuwekeza zaidi katika ufugaji wa samaki, ili idadi ya samaki wanaopatikana kwa njia ya maji ya asili kwa maana ya kwenye Bahari ya Hindi, maziwa na mabwawa iweze pia kupatikana kwa njia ya ufugaji wa kutumia vizimba na mabwawa.
“Tumewaomba kupata utaalamu wao wa ufugaji samaki, lakini pia kama tunaweza kupata wawekezaji kutoka kwao, tuna fursa kubwa na kama wizara tunataka tupate samaki nusu wanaotoka kwenye maji ya asili na nusu wengine wapatikane kwa njia ya kufuga,” amesema.
More Stories
Prof. Mwakalila asisitiza uadilifu, uzalendo kwa wanafunzi wapya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda