Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Zanzibar
BENKI ya NMB imedhamiria kusaidia vijana katika soko la ajira lakini pia kuibua vipaji kutoka vyuoni ambavyo vitakuwa na uwezo wa kukuza uchumi kupitia ajira.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari visiwani Zanzibar, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam na Zanzibar, Donatus Richard amesema benki hiyo imeandaa kongamano maalum katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa lengo la kuwakutanisha wanafunzi wa vyuo vikuu kuzungumza na kuwapa mbinu mbalimbali za ajira na kujiajiri.
“Mbali na huduma mbalimbali ambazo mwanafunzi anaweza kuzipata kupitia NMB, benki pia itamletea elimu maalumu ya masuala ya kifedha, elimu ya akaunti mbalimbali za NMB ambazo mwanafunzi anaweza kufungua na kujiandaa na Maisha baada ya chuo,” amesema Richard.
Aidha kongamano hilo litakaloanza kesho asubuhi, linaitwa ‘NMB Career Fair’ maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vikuu kushirikiana na Benki hiyo ili kutambua fursa mbalimbali ambazo mwanafunzi anaweza kuzipata kupitia benki akiwa mwanafunzi na hata akimaliza chuo.
Richard amesema, NMB ina program nyingi zinazompa nafasi kijana kushiriki kama mfanyakazi, mwanafunzi aliye kwenye mafunzo na pia kuwapa uzoefu wa kazi ili waweze kukidhi vigezo vya uzoefu kazini, hivyo kuweza kufanikiwa vyema kwenye soko la ajira.
“Tuna programu maarufu inayong’amua vipaji vya vijana wanaotoka vyuoni na kuwachukua kuja kufanya kazi kwetu, programu hii inaitwa Management Trainee ambayo mwanafunzi anayechukuliwa anawekwa kwenye uangalizi na kufundishwa mambo mbalimbali na baada ya miaka miwili kama atafanikiwa anapata ajira, kwa miaka mitano iliyopita zaidi ya vijana 50 wameshanufaika na programu hii,” amesisitiza Richard.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu Benki ya NMB, Joanitha Rwegasira amesema: “Kwa tukio la leo tunategemea kukutana na wanafunzi zaidi ya 1000 wanaotoka vyuo vikuu zaidi ya 10 vya hapa Zanzibar. Hii ni mara ya kwanza kwa benki ya NMB kufanya tukio kubwa kama hili linalowakutanisha wanafunzi na wataalam walioko kwenye ajira ili kuzungumza pamoja na kuwapa miongozo ya nini cha kufanya wanapomaliza vyuo na kuingia mitaani katika utafutaji wa ajira.”
Hata hivyo amebainisha kuwa watakaohudhuria wataondoka na zawadi mbalimbali kutoka benki ya NMB na pia watapata elimu nzuri ambayo pengine wasingeipata sehemu nyingine yoyote.
“Sisi kwetu vyuo vikuu ndipo sehemu ambapo tunatoa wataalam wetu na kupitia makongamano kama haya, pia tunaangalia vipaji ambavyo tutaweza kufanya navyo kazi huko mbeleni,” amesema Rwegasira.
Kwa upande wake, Rais wa Tanzania Employment Services Agency, Michael Chacha amesema makongamano ya namna hiyo yanawasaidia wanafunzi kujitambua lakini pia kutengeneza fursa za ajira na pengine kujiajiri.
“Tunawashukuru sana NMB kwa jambo hili kubwa na la kihistoria, wamefika maeneo ambayo sisi hatujafika, makongamano ya namna hii yanawasaidia wanafunzi kujenga uzoefu lakini pia wanajiamini,” amesema Chacha.
NMB ndiyo benki pekee nchini ambayo inawalipa wanafunzi ambao wapo katika ofisi zao kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kabla ya ajira, ambapo kila mwaka wanatoa nafasi kwa wanafunzi zaidi ya 300 ambao hufanya mafunzo kwa vitendo huku wakipewa mikataba ya miezi mitatu hadi 12 ili kuongeza nafasi kwao ya kupata uzoefu wa kazi na hatimaye ajira.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja