November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DCIM\100MEDIA\DJI_0030.JPG

TAWA ilivyodhamiria kuanzisha hifadhi ya kufuga wanyamapori Ruvuma

Na Albano Midelo,TimesMajira online

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akizungumza kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC),aliwaagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kupeleka wanyama kwenye kisiwa cha Lundo ziwa Nyasa wilaya ya Nyasa.

DCIM\100MEDIA\DJI_0030.JPG

Mndeme anasisitiza kuwa kupelekwa kwa wanyama katika kisiwa hicho,kutasaidia kuongeza vivutio kwa watalii kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana wilaya ya Nyasa ambayo imetangazwa kuwa kitovu cha utalii katika Mkoa wa Ruvuma.

Mkuu wa Mkoa pia aliwaagiza wadau wa utalii na uhifadhi wakiwemo TAWA na TANAPA kuchukua jukumu la kutoa elimu ya uhifadhi na utalii kwa wananchi hasa wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu umuhimu wa sekta ya utalii katika kuchochea uchumi.

Mndeme pia ameagiza ushoroba na mapito ya wanyama katika Mkoa wa Ruvuma yaheshimiwe na kulindwa kwa sababu ni moja ya rasilimali za nchi na ameagiza wananchi wote waliovamia maeneo hayo waondolewe haraka.

Kufuatia maagizo hayo wadau wa utalii mkoani Ruvuma wakiwemo TAWA,TANAPA na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) wameanza kuchukua hatua ikiwemo azma ya kuanzisha hifadhi ya kufuga wanyamapori katika kisiwa cha Lundo,kifuga ndege katika kisiwa cha Mbambabay(Zambia).

Mshauri wa Maliasili na Utalii Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema wanatarajia kuanzisha hifadhi ya Mbambabay ambayo inajumuisha visiwa vya Lundo,Mbambabay na milima ya Mbamba,Tumbi na Ndengere wilayani Nyasa.

Challe anaitaja hifadhi ya Mbambabay itakuwa na ukubwa wa eneo la hekta 597 na kwamba maeneo hayo yanafaa kwa kufuga wanyamapori na ndege.

Hata hivyo anasema kati ya hekta hizo,mlima Mbamba una eneo lenye ukubwa wa hekta40,mlima Tumbi hekta 110,kisiwa Mbambabay chenye hekta 27,kitakuwa maalum kwa ufugaji wa ndege na kisiwa cha Lundo chenye ukubwa wa hekta 20,TAWA inatarajia kupeleka wanyamapori jamii ya swala.

“Milima na visiwa hivi vimejaaliwa kuwa na uoto mzuri wa miombo,mawe yanayozunguka visiwa hivi na milima kando kando ya ziwa yana hifadhi samaki adimu wa mapambo zaidi ya aina 400’’,anasisitiza Challe.

Kwa mujibu wa Challe,eneo la hifadhi ya Mbambabay ni muhimu sana kwa upande wa Tanzania hususan katika matumizi ya shughuli za utalii kama vile utalii wa kuvua samaki,kupiga mbizi,yatching, utalii wa kuendesha mitumbwi na kuweka kambi kwenye fukwe.

Mtalaam huyo wa uhifadhi anasema eneo hilo likihifadhiwa litatumika kwa ajili ya mazalia ya samaki na hivyo kuongeza kipato kwa wananchi wanaotegemea shughuli za uvuvi.

“Mbambabay ikihifadhiwa inaweza kuleta ushindani kibiashara hapa nchini kwa sababu katika nchi yetu hakuna eneo linaloweza kutoa mchanganyiko mzuri wa huduma za kitalii kama zitakazotolewa katika eneo hili’’,anasisitiza.

Uchunguzi ulifanywa katika nchi ya Malawi,umebaini kuwa nchi hiyo ina hifadhi kadhaa za Taifa katika ziwa Nyasa.Hifadhi hizo ni pamoja na Lake Malawi National Park na Cape Mcclear Nature Reserve zinazotoa huduma za utalii kwa kutumia rasilimali za ziwa Nyasa.

Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma anasema kutokana na Malawi kupata mafanikio katika ziwa Nyasa upande wa Malawi,mkoa wa Ruvuma unatakiwa kuongeza ubunifu ili kuweza kutoa huduma ambazo ni tofauti na zile zinazotolewa katika nchi ya Malawi.

“Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania ifanye juhudi za kuzitambua huduma zinazotolewa katika hifadhi za Malawi zilizopo ndani ya ziwa na pembezoni mwa ziwa Nyasa’’,anasisitiza Challe.

Kwa mujibu wa Afisa maliasili huyo,maeneo yote yaliopendekezwa kuongezwa katika mradi huo,hayatumiwi katika shughuli za kibinadamu,isipokuwa katika maeneo machache ambayo yanatumiwa na wavuvi kwa kiasi kidogo hivyo kutoathiri hifadhi hiyo mpya.

Mshauri huyo wa Maliasili na Utalii anasisitiza kuwa Kutokana na udogo wa visiwa vya Mbambabay na Lundo,inapendekezwa katika maeneo hayo kusijengwe makazi ya kudumu na kwamba wafanyakazi wa kuhudumia watalii ni vema wawe na makazi nje ya kisiwa ili kuendelea kutunza uoto wa asili uliopo hivi sasa.

“Hii ni hifadhi ya pekee ya wanyamapori pamoja na samaki wa mapambo,itakuwa hifadhi ya ziwa Nyasa ambayo itavutia watalii kufika kusini hivyo kutekeleza Sera ya nchi ya kufungua biashara ya utalii Kusini’’,anasisitiza Challe.

Kwa mujibu wa Challe, hifadhi hiyo itasaidia kulinda mipaka ya Tanzania iliyopo kusini katika ziwa Nyasa na kuitambulisha Dunia kuwa Tanzania inamiliki sehemu ya ziwa Nyasa tofauti na nchi jirani ya Malawi inavyodai.

Challe amepongeza hatua ya Serikali ya Mkoa wa Ruvuma kuagiza milima ya Mbamba,Tumbi na visiwa vya Lundo na Mbambabay kukabidhiwa TAWA ambao hivi sasa ndiyo waliokabidhiwa dhamana ya kutunza hifadhi za wanyamapori kwa niaba ya serikali na wananchi kwa ujumla.

Anasema Idara ya Maliasili na Utalii mkoani Ruvuma wamekusudia kutekeleza azma ya serikali kwa vitendo kwa kuharakisha mchakato wa kukuza biashara ya utalii na kuifanya Mbambabay kuwa kitovu cha utalii katika mkoa wa Ruvuma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Ruvuma alitoa rai kwa Watanzania ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza katika wilaya ya Nyasa ambayo ina vivutio vya kila aina ikiwemo miundombinu bora ya barabara ya lami,meli tatu katika ziwa Nyasa na huduma za kijamii kama umeme zimeboreshwa.

Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 129 kujenga barabara ya lami toka Mbinga hadi Mbambabay wilayani Nyasa yenye urefu wa kilometa 66,pia serikali imetoa zaidi ya bilioni 20 kununua meli tatu katika ziwa Nyasa,Wilaya ya Nyasa sasa imefunguka.