Na Grace Gurisha,TimesMajira,Online Dar
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu wanandoa Twahili na Nadhifa Kopesha, kifungo cha nje mwaka mmoja na kulipa fidia ya sh milioni 15 baada ya kupatika na hatia katika shtaka la kukutwa wakimiliki mihuri 35 ya taasisi mbalimbali za Serikali.
Pamoja na adhabu hiyo, washtakiwa hao tayari wamelipa Serikali fidia hiyo ya sh. milioni 15 kama walivyoingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) pamoja na mshtakiwa mwingine, Nurdin Yusuph.
Adhabu hiyo, imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kassian Matembele wa Mahakama ya Kisutu, ambapo pia alitoa amri ya kutaifisha Euro 6,450 kuwa mali ya Serikali walizokamatwa nazo washtakiwa hao.
Matembele alisema anawapa adhabu hiyo, akizingatia shufaa za washtakiwa kwamba wamekaa gerezani muda mrefu na kwamba ni wakosaji wa mara ya kwanza.
Hakimu pia ametoa amri ya kuharibiwa kwa mihuri hiyo chini ya uangalizi wa Derikali.
Awali, Wakili wa Serikali Faraja Ngukah,akiwasomea hoja za awali washtakiwa hao pamoja na mambo mengine alidai,Septemba 5 mwaka 2019 eneo la Kariakoo Mtaa wa Kongo, mshtakiwa Nurdini na Nadhifa walikamatwa na walipopekuliwa katika makazi yao, zilikamatwa hati zao za kusafiria ikiwemo ya Twahili ambaye ni Raia wa Comoro Mkazi wa Magomeni Kisiwani ambaye ilibainika ni mume wa Nadhifa.
Ilidaiwa kuwa Polisi na washtakiwa hao ,walienda kwa Twahili na alipopekuliwa walikutwa na hati za kusafiria saba za Kitanzania, mihuri 35 ikijumuisha ya Idara ya Uhamiaji Tanzania, Comoro, Zambia, Uganda ya Serikali ya Mtaa Temeke, Kinondoni na Ilala.
Ngukah alitaja vitu vingine vilivyokutwa kuwa ni vyeti vya ndoa, stika za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TPA) na walipohojiwa washtakiwa hao walikiri kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha binadamu.
Ilidaiwa kwamba, washtakiwa hao walikutwa na hati hizo za kusafiria ili ziwasaidie kwenda Italia na Ufaransa wakitoka Tanzania ambapo kila safari iliwagharimu kati ya Euro 300 hadi 640.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â