November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaya, Ofisi za Serikali zazingirwa na maji

Na Israel Mwaisaka,Timesmajira Online. Nkasi

KAYA 320 na Ofisi za Serikali Kata ya Kitanda mwambao mwa Ziwa Tanganyika, hawana makazi baada ya kuzikimbia nyumba zao ambazo zimezingirwa na maji.

Akizungumza na Majira juzi mjini Namanyere Diwani wa Kata ya Kirando, Kakuli Seba amesema nyumba hizo ambazo ni za kisasa zimezingirwa na kujaa maji katika Vijiji vya Mtakuja na Kichangani na kusababisha wananchi kuzikimbia nyumba zao.

“Kila upepo wa Kaskazini unapovuka ujazo wa maji ziwani, unaongezeka na kusababisha mafuriko,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Missana Kwangura amesema tayari viwanja vya makazi vimetengwa na kupimwa jirani na eneo la Shule ya Sekondari Nkasi, ili vigawiwe kwa waathirika wa mafuriko ya maji ya Ziwa Tanganyika.

Amesema eneo hilo liko katika ukanda wa juu, lakini changamoto iliyopo ni mwamko mdogo wa wananchi kuhamia na kujenga makazi yao kutokana na kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii.

Ameongeza kuwa pia Ofisi ya Serikali na mwalo wa samaki umezingirwa na kujaa maji hayo yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.