November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo.

TMDA yabaini dawa bandia ya Mifugo

Na Penina Malundo,Timesmajira,Online

MAMLAKA  ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)  imebaini uwepo wa dawa bandia ya mifugo aina ya Alben Blue 2.5% toleo Na.019394 lililotengezwa mwezi Nov 2019 na lenye tarehe ya mwisho wa matumizi October 2022.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo na Mkurugenzi Mkuu  wa TMDA, Adam Fimbo imesema  mamlaka hiyo kupitia mifumo yake ya ukaguzi  na ufuatiliaji wa bidhaa katika soko iliweza kufatilia na kugundua uwepo wa dawa hiyo bandia.

Imesema dawa hiyo katika lebo yake inaonesha inatengenezwa na kiwanda cha Nerix Pharma kwa niaba ya Vetagro and Pulper Co.Ltd Nairobi nchini Kenya.

Imesema kuwa katika kufanya uchunguzi wa kimaabara ambapo matokeo ya uchunguzi yameonesha kuwa toleo hilo halina kiambata hai.

“Wafanyakazi wote waliokutwa na toleo hili wamefunguliwa mashitaka katika vituo mbalimbali vya polisi na upelezi unaendelea ili kuweza kuutambua mtandao mzima unaojihusisha na utengenezaji ,usambazaji na uuzaji wa toleo hilo bandia la dawa hii,”Imesema

Imesema kutokana na kubainika dawa hiyo,wafugaji wote nchini wanaotumia dawa hiyo kwaajili ya kuua minyoo wanaelekezwa kuangalia kwa makini lebo za dawa hiyo na endapo wataona namba za toleo husika watoe taarifa katika Ofisi zao.