Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online.
IMEELEZWA kuwa upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya nchi ni moja ya hali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Pia upandaji wa miti, inasaidia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa kwa miti dawa ambayo inasaidia kwa kiasi kikubwa jamii kutumia miti hiyo na kujitibu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Shirika la Kijamii la Tanzania Young Women Environmental Conservation Ground (TAYOWEC), Euphrasia Shayo ambapo amesema utunzaji wa miti unafaida nyingi katika maisha ya watu.
Amesema ni vyema watu wakajiwekea mtindo wa kutunza mazingira, ikiwemo kupanda aina mbalimbali ya miti ikiwemo ya dawa ili kuweza kusaidia kuenzi dawa na vyakula vya asili.
Mwenyekiti huyo amesema, dawa za asili na utumiaji wa vyakula vya asili ni moja ya kutunza mazingira na kuimarisha afya.
Shayo amesema kuna umuhimu mkubwa wa watu kutunza mazingira yao na kuhakikisha, wanaenzi na kuthamini vitu vya asili ikiwemo dawa za asili pamoja na vyakula vya asili.
“Kuna umuhimu mkubwa sana wa kutunza mazingira na kuhakikisha jamii inatumia dawa za asili na vyakula vya asili kwa ajili ya kutunza mazingira na kuimarisha afya za miili ya yetu,” amesema na kuongeza;
“Shirika letu limeweza kutekeleza mradi wa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia na kuhifadhi dawa asilia, pamoja na vyakula vya asilia kwa ajili ya kuimarisha afya mradi ambao umefadhiliwa kwa msaada wa Green Grant Fund katika kutoa elimu hiyo mkoani Tanga”.
Amesema katika kutoa elimu hiyo kwenye Mkoa wa Tanga wilayani Muheza, waliweza kutambua zaidi ya dawa 50 kwenye misitu ya Amani na Magoroto chini ya mtaalamu wa dawa za asili, ambapo walipata fursa ya kutoa elimu kwa jamii ya eneo hilo juu ya matumizi ya dawa hizo.
Shayo amesema licha ya eneo hilo kuwa na misitu, lakini wananchi hawakuwa wanajua miti iliyopo katika misitu hiyo kama ni dawa, ambazo zingeweza kuwasaidia pindi watakapougua.
Amesema pia waliweza kuwasaidia wanakijiji wa maeneo hayo, kuanzisha bustani za asili za miti lengo ikiwa ni kujifunza na kuhifadhi miti hiyo ya asili ambayo itawasaidia katika shughuli mbalimbali na kufundishia kwa wanafunzi kujua aina ya miti.
“Tulipata fursa ya kuwafundisha namna ya kupika vyakula vya asili na hii yote ni kusaidia kuwaelimisha juu ya umuhimu wa vyakula asili kwao,” amesema.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa