November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ACT yataka miradi ya kimkakati izidi kupewa kupaumbele

Zitto achambua maeneo 10  ripoti ya CAG

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka watu waache kumshauri Rais Samia Suluhu Hassan, kuacha kuendelea na miradi ya kimkakati iliyoachwa na Hayati Rais John Magufuli, bali anapaswa kuindeleza na kuboresha namna ya utekelezaji wake wa miradi hiyo.

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe

Zitto alitoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusiana na hoja mbalimbali zilizoibuliwa kwenye Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2019/2020 iliyotolewa na CAG, Charles Kichere jijini Dodoma.

Amesema ni vema suala la kuachwa kwa miradi mbalimbali inayoachwa na marais wanaoondoka madarakani isijirudie, bali miradi hiyo iendelezwe, kwani kuiacha kutasababisha hasara kwa miradi ikiyokwisha anza kutekelezwa.

“Maoni yangu ni vema Rais Samia aiendeleze, tutafanya makosa makubwa tukiiacha, kwani huko nyuma tumeona hasara za kuacha miradi mikubwa,”amesema Zitto na  kuongeza;

“Tayari tumeshawekeza pesa nyingi katika miradi mbalimbali mikubwa kama Mradi wa Stiegler’s  Gorge, Mradi wa Reli  na Ndege tukisema tuache hii ni hasara kubwa tutapata na hasara hiyo itaenda kwa nani? Jambo la kufanya ni kuhakikisha tunaboresha namna ya utekelezaji wa miradi na kupunguza madhara.”

Aidha amesema  nchi isirudie makosa ya nyuma ya kila Rais mpya wanapoingia madarakani anakuja na miradi yake na kuacha ile iliyoanzishwa na mtangulizi wake.

“Tusimshauri Rais Samia kurudia haya ya nyuma, tuhakikishe tunamshauri kuendeleza miradi hii ikamilike, lakini ifanyiwe tathimini ni namna gani ya kuboreshwa utekelezaji wake ili iweze kuwa na tija,”amesema

Katika hilo la  utekelezaji Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), Mradi  wa Kuzalisha  Umeme  wa  Maji wa Mwalimu Julius Nyerere maarufu Stigler’s Gorge na ATCL, Zitto amesema Chama hicho kinamshauri  Rais  Samia, kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kujenga mifumo madhubuti ya Uwajibikaji na kuimarisha Taasisi za Uwajibikaji.

“Bila Taasisi imara nchi yetu haitaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo, vinginevyo Miradi mikubwa kama Mradi wa Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, Mradi wa  Reli  ya  Kisasa  na  Mradi  wa  kufufua  Shirika  la  Ndege  la  Taifa  inaweza  kugeuka kuwa miradi  yenye  hasara kubwa kwa Taifa iwapo  hatua  mahususi hazitachukuliwa kuingiza utaalamu, weledi na maarifa katika utekelezaji wake,” amesema Zitto

Ripoti ya CAG

Katika hatua nyingine, Zitto  ametoa ushauri katika maeneo 10 ambapo chama hicho kinatoa mapendekezo ya kuchukuliwa kulingana na hoja zilizoibuliwa  kwenye ripoti ya CAG.

Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa na CAG, Charles Kichere mwishoni mwa wiki, ilianisha madudu mbalimbali ya upigaji fedha za umma, yakihusisha wizara, mashirika ya umma.

Baadhi ya maeneo ambayo CAG alianisha upigaji wa fedha za umma ni Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), akaunti ya Zimamoto kupitisha malipo batili, hasara ya mabilioni ya fedha na ATCL kulemewa mzigo wa madeni pamoja na mikataba mibovu.

Kuhusu TPA

Kuhusu TPA,  Zitto  alishauri CAG  afanye  ukaguzi  maalumu  wa  miradi  yote  mikubwa  inayotekelezwa na TPA, Mamlaka ya Bandari ili kupata uhalisia wa ubadhirifu katika TPA.

“Wakati ukaguzi huo unafanyika tunapendekeza kuwa Mamlaka za Uteuzi zivunje Bodi ya Bandari na kuiunda upya ili kuweza kuweka misingi ya uwajibikaji katika Shirika,” amesema Zitto.

Anashauri madudu Mamlaka ya Bandari (TPA) yachunguzwe zaidi, hasa kwa kuzingatia kwamba  Ripoti  hii  ya CAG imebaini vitendo vya ubadhirifu katika Bandari za Mwanza na Kigoma.

Hata hivyo, Zitto amesema hoja  hiyo  ya  CAG  ni  sehemu  ndogo  sana  ya  ubadhirifu  mkubwa  ambao umekuwa ukifanyika katika Mamlaka ya Bandari Tanzania.

ATCL

Aidha, Zitto alishauri ufanyike ukaguzi wa ununuzi wa Ndege, kubadili muundo wa uendeshaji wa ATCL ili kupunguza hasara.

“Hoja ambayo imeleta mjadala mkubwa katika Ripoti ya CAG ni hasara kwa Shirika la Ndege la Taifa (ATCL). CAG alifanya ukaguzi wa kiutendaji (Startegic and Operational Efficiency)  kwenye  Kampuni  ya  Ndege  Tanzania  na  kubaini  kuwa  Serikali  ilikuwa imetumia sh. Trilioni 1.028 kununua Ndege ili kufufua Shirika la ATCL.

Kati ya Mwaka 2018/19 na  2019/2020 Mapato ghafi  ya Shirika yaliongezeka kutoka sh.  112  bilioni  kwa  mwaka  mpaka  sh.  158  bilioni  kwa  mwaka  sawa  na ongezeko la asilimia 41.

Katika kipindi hicho pia Matumizi ya Shirika yaliongezeka kwa asilimia 45 kutoka sh.  bilioni 134 mpaka sh, bilioni 193. Pamoja  na kununua ndege, kwa miaka mitano  yaani kuanzia 2015/16 hadi  2019/20 Serikali  imeisaidia  Kampuni  ya  Ndege  kiasi  cha  Sh.  Bilioni  153.711  kwa  ajili  ya shughuli  za  uendeshaji  na  maendeleo. 

Fedha  hizi  za  Walipakodi  Serikali  imekuwa ikizitoa kama ruzuku kwa ATCL.

Hata hivyo Shirika limekuwa na hasara ya jumla ya sh. bilioni 153  katika miaka mitano ikiwemo hasara ya sh. bilioni 60.25  mwaka 2019/2020. Ruzuku yote ambayo Serikali imekuwa inadumbukiza ATCL imeliwa na hasara.

“Hata hivyo, Zitto alihoji ilikuwaje CAG hakueleza katika Ripoti yake ilikuwaje Shirika ambalo lina hasara kiasi hicho licha ya Ruzuku ya Serikali liliweza kulipa Gawio kwa Serikali,” amesema Zitto.

Zitto, alishauri CAG afanye ukaguzi Maalumu wa Fedha za Umma sh.  Trilioni 1 zilizotumika kununua ndege.

“Afanye  ukaguzi  wa  usimamizi wa  mkataba  wa  ukodishwaji  wa  ndege  hizo  kati  ya Wakala  wa  Ndege  za  Serikali  na  Shirika  la  Ndege  la  ATCL  ili  Watanzania  wajue matumizi sahihi ya fedha zao za kodi,” amesema Zitto.

“Tunapendekeza  kuwa  CAG  afanye  ukaguzi  wa  manunuzi  ya  Ndege  ili  tuweze kujiridhisha  kama  taratibu  zote  za manunuzi  zilifuatwa  na  nchi  kupata  thamani  ya fedha,” amesema..

Amesema pamoja na hasara iliyobainishwa na CAG kuna matumaini makubwa katika Shirika la ATCL.   “Kinachohitajika  ni maamuzi   sahihi   yenye  maarifa ya sekta husika,” amesema Zito.

Alipendekeza muundo  wa  umiliki  wa  ATCL  ubadilishwe  kwa  kuhusisha mashirika  ya uhifadhi na utalii kama wamiliki.   “Shirika   la TANAPA na  NCAA wamilikishwe  asilimia 60 ya Kampuni na hivyo waondolewe katika orodha ya Mashirika ya kupeleka Hazina asilimia 15 ya Makusanyo yao ghafi,” amesema Zitto.

Aidha, alipendekeza mashirika  haya  ya  Utalii  yaachiwe  kujiendesha  na  kukusanya  mapato  yao wenyewe, asilimia 40 zilizobakia zimilikiwe na Serikali ambapo Kampuni ikikaa vema asilimia 25  ya  Shirika  wamilikishwe  wananchi  kwa  kupitia  Soko  la  Hisa  la  Dar  es  Salaam  ili kuongeza uwazi na kuboresha misingi bora ya uendeshaji wa Kampuni .

Deni la MSD

Katika hatua nyingine Zitto amesema chama hicho  kinapendekeza Serikali ilipe Deni lote la MSD, na pia Serikali itoe mtaji kamilifu kwa MSD  ili  iweze  kujitegemea  kibiashara  katika  shughuli  ya  usambazaji  wa  dawa  kwa wananchi wetu.