November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ndaki amtumbua msimamizi wa mnada Igunga

Na Allan Vicent,TimesMajira Online, Igunga

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amemsimamisha kazi ofisa anayesimamia mnada wa mifugo wa Upili ulioko wilayani Igunga mkoani Tabora, Juma Athuman kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mapato.

Waziri amechukua hatua hiyo juzi alipotembelea mnada huo ili kuangalia ufanisi wake, ambapo alibaini kutokuwepo nyaraka za kumbukumbu ya mifugo inayoingia na kutoka katika mnada huo kwa kipindi cha miaka 4 mfululizo.

Amesema kukosekana kwa kumbukumbu hizo kumetoa mwanya wa upotevu wa mapato ,hivyo kuisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha, hivyo jambo hilo halikubaliki hata kidogo.

‘Naagiza Uongozi wa Halmashauri kumwondoa kazini mara moja Ofisa Afya ya Mifugo, Mohamed Kifamba na askari polisi wote waliokuwa wakisimamia mnada huo nao waondolewe mara moja,” OCD shughulikia hilo’, amesema.

Licha ya kusimamishwa kazi watuhumiwa hao Waziri aliagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina juu ya tuhuma hizo za ubadhirifu wa mapato ya serikali kwa kipindi chote cha miaka 4 ili sheria ichukue mkondo wake.

‘Kila siku ya mnada fedha nyingi zinakusanywa, lakini hazionekani, zinaingia mifukoni mwa watu, hili halikubaliki na Serikali haiwezi kufumbia macho vitendo vya namna hiyo kwa kuwa vinaikosesha mapato mengi sana,” amesema Waziri.

Amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kupeleka wataalamu wilayani humo ili kuchunguza mapato ya mnada huo yaliyopotea katika kipindi chote hicho ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa ikiwemo wahusika kulipa fedha hizo.

Aidha waziri huyo amechukua ya kumkaimisha msamamizi wa mnada huo, Haidari Mwinyihija kuendelea kuungalia mnada huo

Wakati utaratibu wa kumpata ofisa mwingine atakayesimamia mnada huo ukiendelea kufanyika, Waziri alimteua Haidari Mwinyihaji kusimamia mnada huo kwa muda.

Waziri Ndaki amemtaka Mkurungezi wa Halmashauri hiyo kupeleka haraka Mtaalamu mwingine atakayesimamia mifugo katika mnada huo, huku akimtaka OCD wa wilaya hiyo naye kupeleka askari wengine.