November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Spika Ndugai awataka mawaziri walioteuliwa kufanyakazi kwa uadilifu

Na Joyce Kasiki,TimesMajira online,Dodoma

SPIKA wa Bunge Job Ndugai amewata Mawaziri walioteuliwa kufanya kazi
kwa uadilifu katika kuwatumikia wananchi huku akizungumzia suala la
deni la Bohari ya Dawa nchini (MSD) na kutaka deni hilo lichukuliwe na
Wizara ya Fedha na Mipango ili kuokoa maisha ya wananchi wanaokufa kwa
kukosa dawa.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo Bungeni jijini hapa baada ya zoezi
la kuapishwa wabunge watatu ambao ni Balozi Liberata Mulamula,Balozi
Dkt.Bashiru Ally na Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk .

“Kero za wananchi zishughulikiwe ,kwa mfano dawa hakuna na hili siyo
tatizo la leo ,ni la miaka mingi na linajadiliwa kila mara hapa
Bungeni ,kwa nini Wizara ya Fedha msichukue deni la MSD ,kwani si mna
madeni mengi tu mnachukua ninyi ,ili fedha zinazopelekwa MSD zitoe
dawa halafu ninyi mtajuana huko.

“Lakini kila mwaka MSD MSD ,kila wizara kuna mambo ambayo lazima
tutoke huko na wananchi wapate huduma,wananchi wengi wanakufa kwa
kukosa dawa “amesema.

Pia alizungumzia kuhusu upatikanaji wa Bima ya Afya kwa Watanzania
ambapo amesema ,watanzania waliahidiwa upatikanaji wa Bima hiyo katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita .

“ Tulisema Bima ya Afya kwa watanzania wote likashindikana miaka
mitano iliyopita,tumeenda kwenye kampeni tumerudi hilo nalo linahitaji
nini,lazima tuanze nalo ,na tunajua kwa wananchi kipaumbele kikubwa ni
nini kwani tunaishi nao huko, tujitahidi kuwatendea haki watanzania
hawa na tumsaidie Rais .”amesisitiza Spika Ndugai.

Amewataka Mawaziri wote waifanyie kazi dhamana waliyopewa kwa imani
ile ile waliyoaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan aliyewauteua .

“Yapo mengi ya kufanya kila mmoja katika wizara yake na mengi
mtayapata kutoka kwa wabunge cha msingi lazima mjue ninyi ni wabunge
kama sisi,huko mmenda matembezi hapa ndio nyumbani mkiyumba kidogo tu
mmerudi hapa,kwa hiyo tusisahauliane hapa,msisahau kwamba ushauri wa
wabunge ni muhimu sana kwani ndio ushauri wa wananchi.”alisema na
kuongeza.

“Kwa mfano mimi nasikia kila siku wafanyabiashara wakilalamika
,Mawaziri wanaohusika mnahitaji kengele gani igongwe kusema hili jambo
ni kipaumbele namba moja na linahitaji kufanyiwa kazi.”?amehoji Spika
Ndugai.