November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaotoboa ngozi za mifugo kuchukuliwa hatua

Na Severin Blasio,TimesMajira Online,Morogoro

SERIKALI imesema itawachukulia hatua ikiwemo kuwafutia leseni, wachunaji wa ngozi katika machinjio ya Manispaa ya Morogoro wanaotoboa ngozi za mifugo na kuifanya kukosa thamani, licha ya kupatiwa mafunzo na vitendea kazi.

Akizungumza mara baada ya ziara ya kukagua uzalishaji wa ngozi bora zinazohitajika katika soko kaimu mkurugenzi msaidizi wa mazao ya mifugo, usalama wa chakula na lishe,Gabriel Bura amesema licha ya kufanyika mafuzo ya uchunaji bora wa ngozi bado wapo watu wanaokiuta taratibu zilizowekwa.

Bura amesema mafunzo yaliyotolewa, yamesaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa ngozi bora lakini serikali haitawafumbia macho baadhi ya wachunaji wa ngozi wanaoendelea kutoboa ngozi, kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo hasa katika viwanda vikubwa vya ngozi vilivyoanzishwa.

“Tulizitoa lesei hizi kwa sheria ya ngozi namba 18 ya mwaka 2008, pia tulitoa mafunzo ya uchunaji wa ngozi ili kuzipa thamani ngozi mnazozalisha lakini kuna baadhi yenu, bado wanafanya makosa kwa kutoboa ngozi, sasa makosa haya yakijirudia tutawafutia leseni zao,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, imejizatiti kwa kuanzisha na kufufua viwanda nchini kikiwemo kiwanda cha ngozi cha ACE Leather cha Morogoro na kiwanda kama hicho kilichopo Moshi, hivyo kitendo cha kuendelea kutoboa ngozi hizo ni kurudisha nyuma jitihada za serikali.

Amewataka wachunaji hao, kuhakikisha wanaendelea kuzingatia sheria katika utendaji wa kazi zao sambamba na kutengeneza upya leseni zao, ambazo zipo ukingoni kuisha muda wake wa kipindi cha mwaka mmoja ifikapo Agosti mwaka huu.

Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa Nyama Manispaa ya Morogoro, Joseph Kupa amesema wanakabiliwa na changamoto ya baadhi ya watu kushindwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sharia sambamba na magonjwa ya ngozi.

Amesema miongoni mwa changamoto hizo ni baadhi ya wafugaji, kuendelea kupiga chapa mifugo yao jambo linalosabisha ngozi kukosa thamani huku magojwa kama exiima na lab skin, ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakishambulia mifugo.

“Chagamoto tunazopata, mara nyingi ni mifugo kufika machinjioni ikiwa imepigwa chapa na mingine imeshambuliwa na magonjwa ya ngozi, sasa ikifika hapa inakuwa tayari haina thamani hata hatuwezi kuichuna kwa sababu haiwezi kununuliwa na inatokana na baadhi ya wafugaji kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa ngozi,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa wachunaji wa ngozi katika machinjio ya Manispaa ya Morogoro, Mapinduzi Ernest ameshukuru kwa elimu waliyoipata ambayo inawasaidia kwa kiasi kukibwa kuzalisha ngozi bora na kuiomba serikali, kufikisha elimu kwa wafugaji juu ya upigaji chapa ili kubata ngozi bora.