November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU kuongeza nguvu mimba za utotoni

Na Doreen Aloyce,TimesMajira Online,Dodoma

SERIKALI imeitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kuongeza nguvu kwenye kesi za ubakaji na mimba za utotoni ambazo zimekuwa zikiminywa kwenye ngazi za chini na kusababishwa wahanga kukosa haki zao.

Hayo yamesemwa jana jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa TAKUKURU uliowakutanisha wakurugenzi,wakuu wa vitendo na watendaji wakuu.

Akieleza zaidi Ndejembi amesema pamoja na TAKUKURU kushughulikia kesi nyingi na kuwasaidia wanannchi waliodhulumiwa,bado suala la kesi zinazohusu mimba za utotoni linawatesa wanafunzi wengi hali inayowanyima kuendelea na haki ya masomo yao.

“Nategemea na hili mtalimaliza na hatimaye watoto wetu waishi kwa amani bila kudhihakiwa kwenye jamii,ninaamini sana hasa ukizingatia mimi mwenyewe ni mnufaika wa TAKUKURU,bila ninyi kusimamia haki hata leo hii nisingesimama hapa,”amesema Naibu Waziri huyo.

Pamoja na hayo Ndejembi ambaye alijinasibu kuwa mnufaika wa taasisi hiyo yenye dhamana ya kupambana na rushwa amesema ikiwa mapambano ya rushwa ya ngono yatafanikiwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ongezeko la kesi za mimba za utotoni ambazo zimekuwa zikimalizwa kimya kimya.

Kutokana na hayo Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo ameeleza kuwa wao kama watendaji wenye dhamana ya kuisaidia jamii kuondokana na vitendo vya rushwa watahakikisha wanatumia muda wao wote kupambana na waovu wanaokandamiza watu kwa rushwa ya ngono.

Amesema,jamii inahitaji kuishi katika usawa hivyo taasisi hiyo kwa kuzingatia utumishi na utunzaji wa siri watashirikiana bega kwa bega na jamii kuhakikisha uovu wote unaotokana na rushwa unadhibitiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa wa TAKUKURU, Sabina Seja alisema,TAKUKURU kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo itaendelea kusimamia kwa dhati kesi za rushwa ya ngono na kuwapa haki wahanga ambao mara nyingi ni wanafunzi wa vyuo vikuu na mashuleni.

“Tutapambana na kusimamia haki bila upendeo,hadi hali itakapokaa sawa,furaha yetu ni kuona jamii ikishi kwa amani bila vitendo vya rushwa kwa kuwa tunaamini rushwa ni adui wa haki hivyo ili haki itendeke lazima tushughulike na wala rushwa,”amesisitiza Seja.