Na Patrick Mabula , Kahama.
WATU wanaodaiwa wezi wamevunja kioo cha gari la mfanyabiashara Renatus Lucas (44) mkazi wa Mtaa wa Mbulu, mjini Kahama na kuiba silaha aina ya bastola iliyokuwa na risasi 12 na fedha taslimu sh.600,000.
Hata hivyo watu hao walitelekeza bastola hiyo eneo la Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kahama.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba, alisema tukio hilo lilitokea saa nne usiku wakati mfanyabishara huyo alipokuwa ameegesha gari lake nje ya hoteli ya Mary’s Fast Food Hotel iliyopo Phatom mjini Kahama alipokuwa ameenda kula chakula.
Magiligimba alisema, Lucas akiwa ameegesha gari lake aina ya Toyota Clugger namba T 202 DSH nje ya hoteli watu wasiofahamika wanaodaiwa kuwa ni wezi walivunja kioo cha upande wa abiria na kupora bastola na sh.600,000.
Alitaja bastola hiyo kuwa ni aina ya Tisar Maker yenye namba T0620-14J00707 iliyokuwa na risasi 12.
Alisema baada ya Polisi kupata taarifa kutoka kwa mfanyabiashara huyo mara moja walianza kuendesha msako mkali na kufanikiwa kukuta silaha hiyo imetelekezwa na wezi hao eneo la Polisi.
Magiligimba alisema Polisi wanamhoji Lucas kwa tuhuma ya uzembe wa kushindwa kutekeleza wajibu wa kulinda silaha yake na kusababisha kuibiwa.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti