November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ntibazonkiza, Mukoko, Carlinhos kuiongoza Yanga Mapinduzi Cup

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

NYOTA wa klabu ya Yanga Said Ntibazonkiza, Mukoko Tonombe na Carlos Carlinhos watakiongoza kikosi cha klabu hiyo ambacho leo mchana kitaondoka kuelekea visiwani Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi ‘Mapinduz Cup’ itakayoanza kutimua vumbi rasmi kesho.

Wachezaji wengine ambao wamejumuishwa kwenye kikosi hicho cha wachezaji 20 ni kipa Metacha Mnata, Ramadhan Kabwili, Farouk Shikhalo, Adeyum Saleh, Said Makapu, Zawadi Mauya, Kibwana Shomary, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Haruna Niyonzima.

Wengine ni Yacouba Sogne, Tuisila Kisinda, Michael Sarpong, Waziri Junior, Paul Godfrey pamoja na Omara Chibada, Adbilkarim Yunus na Arafat Hussein ambao wamepandishwa kwenye timu kubwa.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesema, kuelekea kwenye michuano hiyo watawakosa wachezaji nane wakiwemo Deus Kaseke, Bakari Mwamnyeto, Yassin Mustapha, Feisal Salum, Ditram Nchimbi na Farid Mussa.

Hafidh alisema kuwa, pia watamkoza Nahodha wao Lamine Moro ambaye ameomba ruhusa kwenda kuona familia yake kwani toka ulipotokea mlipuko wa Covid-19 na mipaka kufungwa hakuweza kusafiri pamoja na Balama Mapinduzi ambaye bado anaendelea na matibabu.

Yanga itatupa karata yake ya kwanza kesho dhidi ya Jamhuri katika mchezo utakaochezwa saa 8:15 Uwanja wa Amaan.