November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miss Tanzania 2020 akutana na watoto wenye matatizo ya usonji

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

MISS Tanzania 2020, Rose Manfere kwa mara ya kwanza tangu kuchaguliwa kwake kutwaa taji hilo amekutana na wazazi pamoja na watoto wenye matatizo ya usonji na kuzungumza nao.

Lengo la kukutana nao ni kusherekea nao sikukuu ya Krismasi na kuwakumbusha wazazi na walezi wa watoto hao kutowaficha ndani badala yake kuwatoa nje ili wawe kama watoto wa kawaida.

Hata hivyo, amesisitiza kukutana na Serikali na kuzungumza nao juu ya kuwasaidia watoto hao hususani katika masuala ya matibabu na elimu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam alipokutana na wazazi na watoto hao, Rose amesema kutokana na masuala ya watoto wenye matatizo ya usonji ni moja ya projecti yake ambayo aliipanga kuifanyia kazi pindi alipoingia katika mashindano ya miss Tanzania hivyo atahakikisha anakuwa balozi mzuri wa watoto hao.

“Nina matumaini makubwa na watu hao wenye matatizo ya usonji naamini nitakuwa balozi mzuri kwao na kuhakikisha nitazungumza na serikali ili watoto hawa wazidi kutengenezewa mazingira mazuri,”amesema Rose.

Aidha amesema, lengo la kukutana na wazazi na watoto hao wenye matatizo ya usonji ni kuwahamasisha wazazi kutowaficha bali kuwatoa nje ili nao wawe kama watoto wengine.

“Nimekuja hapa kutoa elimu na kuhamasisha wazazi wasijisikie vibaya kuwa na watoto hawa na pia kuwatoa watoto hawa nje sio kwenye sinema tu hata katika matukio mbalimbali ili wacheze na watoto wenzao wajisikie kama watu wa kawaida,’’amesema.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Taasisi inayoshughulikia masuala ya usonji kwa watoto, Hilda Nkabe amesema lengo la kuandaa tamasha hilo la watoto wenye matatizo ya usonji ni kutoa elimu kwa wazazi kutowafungia ndani watoto hao na jamii itambue juu ya tatizo hilo na kutowashangaa wanapokutana nao.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Fahamu kwa watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt.Edward Kija amesema kunaumuhimu mkubwa wa kuhakikisha watoto wenye matatizo hayo kutoka katika matukio mbalimbali na kucheza na watoto wenzao.

Amesema, matukio hayo yanawajengea uwezo wa kujiamini, kuwafundisha vitu mbalimbali na kutengeneza mahusiano mazuri baina ya wazazi ili kuona kuwa wananafasi ya kuwatoa watoto hao na kutembea nao.

“Uelewa wa usonji umekuwa unaongezeka mwaka hadi mwaka, tofauti na miaka mitano iliyopita tangu tuanze huduma hizi za kuwatibia watoto hawa uelewa ulikuwa ni mdogo ila kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali pamoja na taasisi mbalimbali zimesaidia uelewa kuzidi kuongezeka,”amesema.