Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KAMPUNI ya Demeter ‘Demeter Insurance Company Ltd’ imefadhili kambi ya timu ya Taifa ya Tanzania ya mchezo wa Kabaddi ya wanawake na wanaume inayotarajiwa kuingia kambini mwishoni mwa wiki kwa ajili ya maandalizi ya awali ya mashindano ya Kabaddi ya Afrika ambayo yamesogezwa mbele hadi Februari 17 hadi 21, 2021.
Katika mashindano hayo ya Afrika mwenyeji Tanzania atawakilishwa na timu ya wanaume na wanawake ambazo zitachuana na timu kutoka nchini Kenya, Cameroon, Egypt, Mauritius, Sirra Leone, Uganda, Afrika Kusini, Nigeria na Zimbabwe lakini pia timu za Uingereza, Malaysia, Taiwan, Iraq na India zilionesha nia ya kuja kama waalikwa ingawa ushiriki wao utategemea maamuzi ya bodi ya Kabaddi Afrika (Africa Kabaddi Federation na World Kabaddi).
Awali timu hiyo ilitakiwa kuingia kambini mwanzoni mwa mwezi uliopita chini ya makocha wa kimataifa wa mchezo wa Kabaddi kutoka nchini India, Amrik Singh na Vijender Singh ambao wangeshirikiana na makocha wa hapa nchini.
Lakini kabla ya makocha hao kutua hapa nchini kwa ajili ya mashindano hayo yaliyopangwa kuanda Desemba 11 hadi 15, Africa Kabaddi walitangaza kuyaahirisha kutokana na baadhi ya nchi kushindwa kuthibitisha kutokana na kuendelea kukabiliwa na ugonjwa wa Corona.
Licha ya mashindano hayo kuahirisha lakini nchi wanachama zitakazoshiriki mashindano hayo zimetakiwa kuwasilisha majina na nakala za hati ya kusafiria za wajumbe wao kabla ya Desemba 31, 2020.
Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo cha Kabaddi Tanzania (TKSA) Abdallah Nyoni amesema, timu hiyo itaingia kambini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya awali ambapo kambi hiyo imefadhiliwa na Adarsh K. Sharma ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Demeter Insurance Company Ltd.
Kikosi hicho kitakachoingia kambini kitakuwa chini ya kocha Sharma kutoka Indian School atakayesaidiana na makocha wengine na hadi sasa tayari kampuni hiyo imeshaanza maandalizi muhimu ya kuanza kambi ikiwemo kununua vyakula kwa ajili ya wachezaji na mahitaji mengine muhimu.
Hata hivyo kiongozi huyo amesema kuwa, huenda kikosi kitakachoingia kambini kikawa na mabadiliko kutokana na kupunguza na kuongeza majina ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wao.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo ameweka wazi kuwa, wapo mbioni kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Mkuu wa Mkoa ambaye amekubali kukutana nao kwa ajili ya kufanya mazungumzo na kuweka mikakati ya mashindano hayo ya Afrika ambayo Tanzania ni mwenyeji.
Pia wamepanga kuangalia namna ya kuunganisha Serikali mbili (Tanzania na India) ili kuimarisha mchezo huo hapa nchini na kutekeleza mkakati wao wa kufanya mchezo huo kuchezwa nchi nzima.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship