November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAMWA yazungumzia matukio ukatili wa kijinsia

Na Penina Malundo,TimesMajira Online.

CHAMA cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimesema licha ya vyombo vya dola kuchukua hatua mbalimbali katika ukatili wa kijinsia, lakini matukio ya ubakaji, ulawiti, mimba katika umri mdogo na udhalikishaji bado vipo nchini.

Pia kimeitaka jamii kuhakikisha inafichua ukatili unaofanyika katika maeneo yao, ili kuleta mabadiliko kwenye jamii katika kupinga ukatili wa kijinsia nchini.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa TAMWA, Rose Reuben wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Duniani amesema, endapo jamii itafumbia macho na kuyakalia kimya matukio ya ukatili, suluhisho halitapatikana.

Rose amesema TAMWA, Kituo cha Usuluhishi cha Huduma ya Ushauri na Nasaha (CRC) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani nchini (UsEmbassyTz), wameungana kwa pamoja katika maadhimisho hayo katika kuwasisitiza wananchi kuibua na kufichua matukio ya ukatili wa kijinsia yanavyotokea.

“Siku hii inaadhimishwa duniani kote, wakati Tanzania ikiwa bado na matukio mbalimbali ya ubakaji, vipigo, rushwa ya ngono, udhalilishaji, ndoa na mimba za utoto ambapo kauli mbinu ya maadhimisho haya ni ‘Pinga ukatili wa kijinsia, mabadiliko yanaanza na wewe’,” amesema na kuongeza;

“TAMWA imefanya jitihada za kupunguza ukatili wa kijinsia chini ya miradi yake mbalimbali, ikiwemo wa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi unaofadhiliwa na African Women Development Fund (AWDF) na ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wanawake, (UN-Women)”.

Amesema chama chao kinaibua matukio mbalimbali ya ukatili yanayoweza kutokea katika nyanja za siasa na uongozi kazini hivyo hukaa na wadau hao.

“Mafanikio ni makubwa lakini bado jamii inatakiwa ishike hatamu kwa kuvunja ukimya na wakati huo, wanaharakati na serikali nao watimize wajibu wao, kufanya hivyo tutapunguza tatizo hili,” amesema.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Marekani, Dkt. Willow Williamson amesema ubalozi wake umekuwa ukisaidia taasisi mbalimbali katika programu za masuala ya elimu, afya na ukatili wa kijinsia na kufanikisha takribani walimu 1,500 na wanafunzi 4,000 katika programu mbalimbali.

Amesema kwa kushirikiana na TAMWA kwa pamoja, wataleta mabadiliko na kubadili mtazamo wa jamii katika masuala ya ukatili wa kijinsia kwa jamii.

Naye Mwakilishi wa CRC, Gladness Munuo amesema lengo la kituo chao ni kumaliza kesi mezani zinazowakabili watu mbalimbali.

Amesema kesi kubwa zinazowafikia katika kituo hicho ni pamoja na wazazi upande mmoja kuwatelekeza watoto, kesi upande wa ndoa pamoja na kesi za mirathi hususan kwa wanawake.

Munuo amesema ndani ya kipindi cha miaka 10 wameweza kufanikiwa kusuluhisha kesi nyingi huku zilizomalizika kabisa zikiwa kesi 25.

“Mara nyingi kituo chetu vinatoka elimu,ushauri,nasaha na msaada wa kisheria pindi watu wanapokuwa hawaelewani au kuna hali ya ugomvi,” amesema na kuongeza;

“Wakati mwingine tunawasapoti kiuchumi katika kuwapatia mitaji hasa kwa wale wanaotelekezwa katika kuwainua kiuchumi”.