November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Enock: Msiache ARVs kwa madai ya kuombewa, kuokoka

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

WATU walioambukizwa Virusi vya UKIMWI (VVU) na wenye maradhi ya UKIMWI walioanzishiwa dozi ya ARVs na baadaye kuamua kuokoka, wameshauriwa kutokatiza dozi zao kwa imani ya wokovu, kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwasababishia madhara zaidi kiafya, kabla ya kufikiwa na uponyaji wa Mungu.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika ibada mbalimbali kanisani Karmeli Deliverance Ministry International (KDMI), Tangibovu-Mbezi Beach, Dar es Salaam hivi karibuni, Mchungaji na Nabii Dkt. Enock Mwasambogo, amesema kutupa ARVs ni imani iliyopita kiasi, ambayo, kama mwonaji na mshauri wa kiroho hamuungi mgonjwa yeyote kuivaa hata kama ameokoka.

Kwa mujibu wa Dkt. Enock, ARVs haziwezi kumponya mwenye UKIMWI wala kumuondolea VVU aliyeambukizwa, bali zinampunguzia makali ya maradhi hayo na kumfanya aonekane mwenye afya na matumaini wakati wote anapokuwa kwenye maombi akiutafuta uponyaji wa Mungu.

Dkt. Enock amesema; “Ukimwona mgonjwa wa UKIMWI aliyeokoka anatupa ARVs zake wakati hajapokea uponyaji mwambie asiige yasiyoigwa, na wala asijaribu kuonesha kuwa na imani zaidi hata ya Yesu mwenyewe.

Amesema kwa sababu wakati wa uponyaji unaamuliwa na Mungu mwenyewe kwa kadri apendavyo, mtu kutamka kuwa ameokoka, kuhudhuria kanisani kwenye maombi na maombezi na kuamini katika miujiza ya uponyaji hakumaanishi kuwa ni lazima apone muda huo.

Kutokana na ukweli huo, amesema ili mgonjwa asijishindwe kwa kuchoka mwili kutokana na kukongoroka na pengine kushindwa kumaliza safari ya kuutafuta uponyaji kanisani ni vyema akaendelea kumeza dawa zake kwa utaratibu ufaao na si kuruka dozi.

“Hakuna mahali Mungu alipokataza watu waliookoka wasiende hospitali au wasitibiwe, ndio maana tunahubiri na kuwashauri wagonjwa wanaokuja kanisani wahakikishe hawapuuzi ushauri wa madaktari wakati uponyaji wa Mungu ukiendelea.”

“Wengi wanakufa kwa imani ambazo hata Mungu mwenyewe haziungi mkono. Una malaria, unapewa dawa kunywa umalize dozi usitupe eti kwa kuwa umeokoka, ukicheza utakufa na tutakuzika,”alisema na kuongeza kuwa mambo ya rohoni yafanyiwe kazi kiroho na ya mwilini yafanyiwe kazi kwa njia bora za mwilini ili Mungu naye ayabariki.