October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TFF: Kushughulikia suala la Kabwili ni kuvuruga uchunguzi

Na Mwandishi Wetu

SAA chache baaada ya Uongozi wa klabu Yanga kulitaka Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutoa majibu ya kesi walizowawasilishia mezani, Shirikisho hilo limeweka wazi kuwa, kwa sasa ni ngumu kushughulikia suala hilo hasa la madai ya kipa wao, Ramadhan Kabwili kwani ni kuvuruga uchunguzi.

Jana Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema, TFF inapaswa kutoa majibu ya ya kesi zao mbili ikiwemo ya golikipa huyo pamoja na ile ya Benard Morrison ambazo zipo kimya kwa muda mrefu.

Amesema, wao kama klabu hawana hawana tatizo lolote na TFF, lakini wanashangaa kuona kesi zao zikichelewa kutolewa majibu licha ya muda kupita sana toka walipopeleka madai yao .

Mwakalebela amesema kuwa, kesi ya Kabwili waliipeleka hadi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na tayari majibu yalishatolewa kwani hata wao waliyapata pia.

“Yanga tuliwasilisha malalamiko TFF kuhusu tuhuma za rushwa za kipa wetu ambaye alikuwa akishawishiwa na viongozi wa wapinzani ili kuihujumu Yanga, tulifikisha malalamiko yetu TFF na Takukuru hivyo TFF wanatakiwa kutoa majibu wamefikia wapi kwani Takukuru walitoa ushirikiano mkubwa,” amesema Mwakalebela.

Lakini kuhusu suala la kesi ya aliyekuwa mchezaji wao Benard Morrison, kiongozi huyo amesema kuwa, walishaweka wazi kuwa, mkataba wake uliopo kwa sasa sio sahihi na kuomba ufafanuzi kutoka TFFlakini pia hadi sasa bado wapo kimya.

Amewema, wao kama klabu wameingia wasiwasi kuwa huenda kuna njama zinafanywa kuchelewesha jambo hilo ili dirisha dogo likifunguliwa waweke mkataba mwingine.

Kutokana na madai hayo, TFF wamesema kuwa, taarifa za kuwa imekalia kesi kuhusu tuhuma za madai ya upangaji matokeo zilizotolewa na Kabwili ni upotoshaji.

Taarifa iliyotolewa na cliford Ndimbo imesema kuwa, madai yaliyotolewa na kabwili kuhusu upangani wa matokeo yanachunguzwa na vyombo vya kisheria vya nchi hivyo kwa kuzingatia weledi, hawawezi kushughulikia madai hayo katika utaratibu wake kwani ni kuvuruga uchunguzi unaoendelea kuhusiana na jambu hilo.

Pia TFF wamesisitiza kuwa, watasimamia, kuendesha na kuratibu shughuli za soka kwa mujibu wa Katiba, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali iliyotolewa na shirikisho la Soka ulimwenguni (FIFA).