October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Mndeme kufungua mafunzo ya Gasshuku 2020

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa semina ya mchezo wa Karate (Gasshuku 2020) yatakayofanyikia Songea Mkoani Ruvuma kuanzia Desemba 4 hadi 6 mwaka huu.

Semina hiyo ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka katika Mikoa mbalimbali, mwaka jana ilifanyikia katika Mkoa wa Morogoro na safari hii kupelekwa Ruvuma lengo kuu likiwa ni kuangalia viwango vya makarateka hapa nchini.

Uongozi wa Chama cha Mchezo wa Karate Tanzania JKA/WF-TZ chini ya Mkufunzi Mkuu wa Karate Tanzani (J.K.A), Jerome Mhagama umeweka wazi kuwa, tayari ulishaanza maandalizi ya semina hiyo ya siku tatu itakayohusisha watu wa kada mbalimbali wakiwemo walimu na wanafunzi.

Amesema kuwa, ujumbe mkuu katika mafunzo hayo ni kuhamasishana na kufanyia tathmini ya viwango vyao vya Karate ikiwemo kutengeneza ujirani mwema baina ya klabu moja na nyingine.

Mkufunzi huyo amesema kuwa, hadi sasa klabu mbalimbali zimeshathibitisha kushiriki mashindano hayo huku pia wakiendelea na maandalizi ikiwemo kuzihamashisha zaidi klabu nyingine kujiunga na kushiriki mafunzo hayo kwani hayatakuwa na kiingilio.

Sababu kubwa za kufanyia mafunzo hayo Ruvuma ni kuhamasisha kuundwa kwa klabu mbalimbali za mchezo huo na kuhamasisha jamii kupenda Karate.

“Sisi kama Makarateka kutoka klabu zote Tanzania, tutakutana katika mafunzo haya ya pamoja ambayo tunatarajia mgeni rasmi atakuwa RC Mndeme tukilenga kuelimishana mambo mbalimbali yanayohusu taaluma yetu ikiwemo kufanya tathmini ya viwango vyetu, ” amesema Mhagama.