Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo kitakuwa na kibarua katika uwanja wa Benjamin Mkapa kuwakabili wapinzani wao Tunisia katika mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2021) utakaochezwa saa 4:00 usiku.
Tanzania itaingia katika mchezo huo huku ikitaka kubadili matokeo baada ya kupoteza kwa goli 1-0 mchezo wa awali uliochezwa Novemba 13 katika uwanja wa Stade Olmpique de Rades uliopi Tunis.
Mchezo huo utaamuliwa na waamuzi kutoka nchini Msumbiji ambapo mwamuzi wa kati atakuwa Celso Armindo Alvacado akisadiwa na mwamuzi wasaidizi namba moja Arsenio Chadreque Marengula, mwamuzi msaidizi namba mbili ni Zacarias Horacio Baloi huku mwamuzi wa akiba akiwa Simoes Bernardo Guambe .
Kamishna wa mchezo Diamini Zide Gilbert anatokeo nchini Eswatini huku Mtathmini waamuzi Mfubusa Bernard akitokea nchini Burundi.
Katika mchezo wa awali waliocheza kwenye uwanja wa Stade Olmpique de Rades timu hizo zilicheza bila mashabiki lakini hapa nchini Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) limeruhusu mashabiki huku wakielekeza kuwa idadi ya watakaoingia ni asilimia 50 yauwezo wa uwanja.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Etienne Ndayiragije ameweka wazi kuwa, mbali na Nahodha wa timu hiyo Mbwana Samatta kukosekana ndani ya kikosi toka mchezo wa awali lakini pia kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ hatokuwa sehemu ya mchezo huo baada ya kupata majeraha katika mchezo wao wa awali uliochezwa Novemba 13.
Licha ya kukosekana kwa wachezaji hao lakini bado wanamatumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mchezo huo wa nyumbani kwani tayari ameshafanyia kazi makosa yaliyowagharimu katika mchezo wa awali lakini pia ana wachezaji wazuri ambao wanauwezo wa kuamua matokeo.
Amesema, safari hii wapo nyumbani tena mbele ya mashabiki wao hivyo wana uwezo wa kucheza kwa kujimini na kupata matokeo bora kwani tayari kila mmoja amekubali kujitoa mhanga ili kuipeperusha vema bendera ya Taifa nyumbani.
“Tutaingia katika mchezo wetu wa leo kwa kujimini lakini kucheza kwa heshima kutoka na ubora wa wapinzani wetu ili kufikia malengo yetu kwani kama timu tumeamua kuwa tunakwenda kubeba bendera ya Taifa hivyo ni lazima kujitoa kwa hali na mali ili kufikia malengo yetu, ” amesema Ndayiragije.
Jana Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Yusuph Singo alieleza kuwa, wao kama serikali watahakikisha maagizo yote yaliyotolewa na CAF yanazingatiwa katika mchezo wa leo na tayari walishatoa maelekezo kwa wauzaji wa tiketi kuzingatia idadi ya tiketi zitakazouzwa.
Pia Singo amewataka mashabiki hao kuzingatia umbali wa mita moja kama ilivyoelekezwa kwani ikiwa agizo hilo litakiukwa huen da ikaleta athari na pengine hata mechi zijazo za ligi mabingwa pamoja na Shirikisho zikachezwa bila mshabiki.
“Kama tunavyojua Caf wameshatoa maelekezo na kwa upande wetu tumeshatoa muongozo kwa wauzaji wa tiketi na sasa kazi kubwa ipo kwa mashabiki kuzingatia kukaa umbali za mita moja au zaidi ili kutoleta athari katika mechi zijazo za kimataifa, ” amesema Singo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, ameeleza kuwa, walipambana kuomba kubadilishiwa muda wa mechi lakini CAF waligoma kulingana na sababu kadhaa ikiwemo ya wenye haki ya kurusha mechi hizo.
“Baada ya kupambana na kuruhusiwa kuingiza mashabiki bado tuliendelea kupambana ili mchezo urudishwe nyuma tukitoa sababu ya usala kwani hatujawahi kucheza mechi muda huo lakini tukaambiwa kuwa kama uwasala ni mdogo basi watazamaji watakaoruhusuwa ni asilimia 25 na baada ya kuona hivyo tuliona bora tuache mchezo uchezwe muda ule ule kwani pia Caf walituambia hawawezi kurudisha mchezo nyuma kutokana na sababu kadhaa iliwemo wenye haki ya matangazo ya televisheni,” amesema Kidao.
Isikie Kamati ya Hamasa
Kuelekea katika mchezo huo, Kamati ya Hamasa ya Taifa Stars imewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu hiyo kwani wao tayari wameshafanya jitihada kubwa kuhakikisha timu hiyo inachukua alama tatu katika uwanja wa nyumbani.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Mhandisi Hersi Said pamoja na Mkuu wa Kitendo cha Idara ya Habari ya Simba, Haji Manara ambao ni sehemu ya viongozi wa Kamati hiyo wamewataka wanachama na mashabiki wa klabu hizo mbili kuungana kuishangilia Stars itakapokuwa inacheza mechi hiyo muhimu.
“Tuache kuweka matabaka yasiyokuwa na tija, tuzipende timu zetu lakini tutambue kuwa zote hizo Mzazi wake ni Tanzania, inapokuwa inacheza Stars inamaanisha ni suala la nchi sio timu hizi mbili pekee, kwahiyo mashabiki wa Yanga na Simba wajitokeze uwanjani na washangilie bila kuwepo matabaka,” amesema Injinia Hersi.
Kwa upande wake Manara amesema kuwa, “Kitu cha kwanza cha kuzingatia ni utaifa, sisi ni Watanzania, Simba na Yanga zile sio nchi ni klabu, hauwezi kwenda nje ya Tanzania ukaulizwa unatoka wapi ukajibu Yanga au Simba lazima uitaje Tanzania hivyo kwa pamoja kesho tuvae jezi za Stars tuingie uwanjani kuwashangilia vijana wetu,”.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025