October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwakinyo: Sitowaangusha, Paz aahidi shoo ya kibabe

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

BONDIA wa Kimataifa wa Tanzania anayeshikilia ubingwa wa Mabara wa WBF uzito wa Super Welter, Hassan Mwakinyo kesho usiku anapanda ulingoni kutetea ubingwa wake wa Mabara katika pambano la raundi 12 dhidi ya mpinzani wake Jose Carlos Paz kutoka Argentina.

Pambano hilo la kimataifa litasimamiwa na rais wa Chama cha Ngumi za Kulipwa cha WBF, Howard Goldberg huku mwamuzi maarufu duniani, Edward Marshall akiaminiwa kuchezesha pambano hilo.

Pia pambano hilo la ubingwa litasindikizwa na mapambano yatakayowakutanisha nyota wa nchi tano tofauti ikiwemo Mtanzania, Hussein Itaba atakayezichapa na Alex Kabangu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DR Congo), Fatuma Zarika wa Kenya ataonyeshana kazi na Patience Mastara wa Zimbabwe huku Mwanadada Zulfa Macho akizichapa na Alice Mbewe wa Zambia.

Akizungumza mara baada ya kupima uzito, Mwakinyo amesema, anajua kuwa Paz ni bondia mzuri lakini hatotamba kwake kwani amejiandaa vyema kuelekea pambano hilo ili kuwapa furaha Watanzania.

Mipango yake ni kuhakikisha anamtwanga kwa ‘Technical Knock out (TKO)’ mpinzani wake tena katika raundi za mwanzoni ili kumaliza utata.

“Nataka kufanya staili ya mabondia wa zamani kama Mike Tyson ambaye alikuwa anamaliza pambano huku mashabiki wakiwa katika foleni ya kuingia na wengine wakikata tiketi. Nawaomba mashabiki wa ngumi za kulipwa nchini, kuwahi kukata tiketi na kuwahi kuingia ili kushuhudia nikiweka historia nyingine tena ndani ya nchi yangu,” amesema Mwakinyo.

Mwakinyo amesema kuwa, atahakikisha kipigo atakachompa Paz kitamfanya aamue kuachana na mchezo wa ngumi za kulipwa .

“Ninachoongea ndicho ninakimaanisha, nataka kuonyesha mimi ni bondia wa iana gani katika familia yetu ambayo mchezo wa ngumi na kickboxing ni moja ya shughuli zake, sina mchezo katika pambano hili, lakini pia sitadharau mpinzani wangu” amesema.

Lakini kwa upande wake Paz amesema kuwa, amejipanga kucheza mchezo mzuri ambao utawafanya Wanzania kufurahia na kuzidi kuupenda mchezo huo na atahakikisha mikono yake ndiyo ‘inaongea’ ulingoni ili kuthibitisha ubora wake.

Kwa upande wake Rais wa WBF, Howard Goldberg amesema, maandalizi yamekamilika na endapo Mwakinyo atashinda pambano hilo, atapata nafasi ya kuwania ubingwa wa dunia dhidi ya bingwa mtetezi, Lasha Gurguliani wa Georgia ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

“Napenda kuwashukuru kampuni ya Jackson Group Sport kwa kuandaa pambano hili na kurejesha thamani ya ngumi za kulipwa nchini. Hii ni mara yangu ya saba kuja nchini, lakini sijawahi kushuhudia weledi wa aina hii katika kuandaa pambano,” amesema Goldberg.

Mkurugenzi wa kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa amesema kuwa, maandalizi yamekamilika na kwa mara ya kwanza Tanzania inawakutanisha mabondia kutoka nchi nyingine tano duniani na kuweka historia.