October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Moja ya hafla za utoaji vyeti na leseni kwa wazalishaji waliokidhi matakwa ya viwango. Picha na Maktaba

TBS yawataka walizalishaji kuingatia ubora

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji waliopatiwa leseni na vyeti vya ubora kuwa mabalozi wazuri katika matumizi ya viwango ili kufikia lengo la Tanzania ya viwanda hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania ipo katika uchumi wa kati.

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya kwenye hafla ya utoaji vyeti na leseni kwa wazalishaji ambao bidhaa zao zimekidhi matakwa ya viwango.

“Muendelee kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango kwa mustakabali wa afya na mazingira ya watumiaji kwa ujumla,” amesema Dkt. Ngenya.

Ameongeza kwamba leseni na vyeti vilivyotolewa mwishoni mwa wiki vitazisaidia bidhaa zilizothibitishwa kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kushindana sokoni, kuondoa usumbufu wa kupima bidhaa kwa kuzingatia matakwa ya mnunuzi.

Aidha, amesema vyeti na leseni hizo zitasaidia mzalishaji dhidi ya ushindani na bidhaa duni,hafifu zisizo na ubora, kuongeza imani kwa umma juu ya ubora wa bidhaa iliyothibitishwa hivyo kumpatia wateja zaidi.

“Vyeti na leseni hizi zitawawezesha wazalishaji kuingia na kuuzwa katika soko la Afrika Mashariki pasipo kufanyiwa vipimo zaidi,” alisema.

Kwa upande wa mlaji na watumiaji, Dkt. Ngenya amesema vyeti na leseni hizo zinamthibitishia kuwa bidhaa husika inafaa kwa matumizi husika.

“Kumhakikishia usalama wake kiafya na pia katika matumizi na kulinda mazingira,” amesema.

Hivyo natoa pongezi kwa wazalishaji wakubwa, wa kati pamoja na wajasiriamali wadogo waliofanikiwa kupata vyeti na leseni za kutumia alama ya ubora.

Kwa mujibu wa Dkt. Ngenya wazalishaji hao bidhaa zao zimethibitishwa ubora baada ya kukidhi matakwa ya viwango kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba, 2020 ambapo vyeti na leseni zilizotolewa ni 177.

Amesema kati ya hizo, leseni 1 ni ya mfumo wa usimamizi ubora, leseni 146 za alama ya ubora na 30 ni vyeti kwa bidhaa zisizo na viwango vya Tanzania.

Aidha, kati ya leseni na vyeti vilivyotolewa, alisema 88 ni vya wajasiriamali wadogo. “Vyeti na leseni hizo ni za bidhaa za vyakula, vipodozi, vifaa vya ujenzi, vilainishi, vitakasa mikono, vifaa vya umeme, vifaa vya makenika, magodoro, vibebeo pamoja na vifungashio.

“Naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na John Magufuli kwa kuwahudumia wajasiriamali wadogo kupitia huduma za TBS juu ya uthibiti ubora bila malipo ya gharama za ukaguzi na upimaji.

Wajasiriamali wadogo hawa wataendelea kuhudumiwa bure kwa kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo. Hata baada ya miaka mitatu kuisha, TBS itafanya tathmini ya uwezo wa wajasiriamali ili kupima uwezo wao wa kulipa,” amesema Dkt. Ngenya.

Hivyo alisema ni muhimu kwa wajasiriamali kuhifadhi vizuri kumbukumbu za uzalishaji na mauzo ili visaidie katika zoezi la tathmini.