October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Takwimu magonjwa yasiyoambukiza zinatisha Dar

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Dar es Salaam

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge amesema takwimu za magonjwa yasiyoambukiza zinatisha, zikionesha tatizo hilo ni kubwa na kuwataka viongozi na Watanzania wote kulipa umuhimu unaostahili ili kulikabili.

Aidha, ameagiza maofisa ustawi wa jamii ngazi zote wawezeshwe kwa kupewa mafunzo ili wasaidie kuelimisha wananchi maeneo yote kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Ametoa kauli hiyo jijini humo wakati akizindua maadhimisho ya Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza, ambayo kitaifa yanafanyika jijini Dar es Salaam, huku akieleza kutoridhishwa kwake na ushiriki wa viongozi katika uzinduzi huo.

“Nasikitika ushiriki wa viongozi. Sijafarijika sana na hili. Sijaridhishwa na ushiriki hasa wa watu wenye nafasi ya kufanya maamuzi.

Takwimu za magonjwa haya zinaonyesha ipo shida, hivyo suala hili lazima lipewe umuhimu unaostahili. Serikali imefanya jitihada na kuelekeza itengwe siku ya mazoezi,” amesema na kongeza:

“Naagiza katika mipango miji tuhakikishe kunakuwa na maeneo ya mazoezi ya watoto na tuyaendeleze, yasivamiwe. Taasisi ziwezeshe mazoezi, pia maofisa ustawi wa jamii wapewe mafunzo, wasaidie kuelimisha ngazi zote za jamii kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.”

Mazoezi ya viungo

Awali, akitoa takwimu, Naibu Mkurugenzi anayeshughulikia magoinjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Grace Magembe, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alisema katika miaka minane iliyopita magonjwa hayo yameongezeka na yanachangia idadi kubwa ya vifo vya watanzania.

“Katika miaka minane iliyopita magonjwa yasiyoambukiza yameongezeka, sasa yanachangia asilimia 35 ya vifo vya watu. Magonjwa hayo ni pamoja na kisukari, moyo, figo, magonjwa ya mfumo wa hewa, saratani na ajali,” amesema.

Alibainisha kuwa: “Kibaya zaidi, iliaminika magonjwa hayo ni ya watu wazima pekee, lakini sas hata vijana wanaugua, lakini habari nzuri, yanazuilika na hayahitaji mamilioni ya fedha kuyazuia. Ili kuyakabili ni lazima kubadili mtindo wa maisha kwa kufuata kanuni bora za ulaji.”

Alitaja baadhi ya viashiria na sababu za magonjwa hayo kuwa ni pamoja na kuwa na uzito kupita kiasi, matumizi ya chumvi na sukari kupita kiasi na kutofanya mazoezi.

Tukio hilo lilitanguliwa na washiriki kufanya mazoezi katika viwanja vya Leaders yaliyofuatiwa na maandamano kutoka eneo hilo hadi viwanja vya Mnazi mmoja, ambao uzinduzi ulifanyika, kabla ya Mkuu wa mkoa wa dar es Salaam kuzindua michezo kwa ajili ya wiki hiyo katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Park, zamani Kidongo Chekundu.

Maadhimisho hayo yaliyoanza Novemba 7 yanaendelea kwa shughuli mbalimbali, ambapo leo na kesho litafanyika kongamano la kitaaluma katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere, ambapo watajadili na kutoa mwelekeo wa mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Novemba 11 wananchi watapewa fursa ya kupima magonjwa hayo na ushauri viwanja vya Mnazi Mmoja utakaoendelea sanjari na maonesho yatakayoanza Novemba 12 hadi 14 yakijumuisha Shirikisho la Vyama Vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), Wizara ya Afya, Maendeleo ya JAmii, Jinsia na Watoto na wadau wengine.