October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Diego Maradona

Diego Maradona afanyiwa upasuaji wa Ubongo

BUENOS AIRES, Argentina

NYOTA wa zamani wa mpira wa miguu Duniani, Diego Maradona amefanyiwa upasuaji wa ubongo juzi, kwenye Kliniki ya Olivos huko Buenos Aries, Argentina na kwa sasa hali yake inaendelea vizuri.

Maradona, mwenye umri wa miaka 60 raia wa Argentina, alilazwa kliniki ya Ipensa huko La Plata, Argentina siku ya Jumatatu huku akiugua upungufu wa damu na kujaa maji mwilini.

Hata hivyo, nyota huyo baadaye alihamishiwa kwenye Kliniki ya Olivos huko Buenos Aries ili kufanyiwa upasuaji kwenye hematoma ambapo kulikuwa na mkusanyiko wa damu kati ya utando na ubongo wake.

Akizungumzia hilo, Dkt. wa Maradona Leopoldo Luque amesema, amemfanyia upasuaji nyota huyo kwa kwa mafanikio makubwa na alikuwa mvumilivu sana.

“Hatua ya sasa ni uchunguzi na itategemea jinsi hali itakavyokuwa ingawa sio ngumu sana, lakini kutafanyika upasuaji mwingine wa ubongo,” amesema daktari huyo.

Maradona, ambaye alishinda Kombe la Dunia mwaka 1986, akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Argentina, anachukuliwa kuwa mmoja wa wachezaji bora na wakubwa wakati wote duniani.

Kocha huyo wa Gimnasia Esgrima, mara ya mwisho alionekana hadharani katika siku yake ya kuzaliwa siku ya Ijumaa iliyopita kabla ya mechi ya ligi ya timu yake dhidi ya Patronato.