October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sonona hukosesha hamu tendo la ndoa-Daktari

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira,Online, Dar

MSONGO wa mawazo pamoja na sonona ni miongoni mwa dalili za tatizo la afya ya akili ambalo huchangia mtu kukosa hamu ya kula pamoja na tendo la ndoa.

Hayo yamesemwa na Daktari wa Magonjwa ya Akili, Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili (MUHAS), Dkt Isaak Lema wakati wa mafunzo maalumu kwa watu wanaougua Magonjwa Yasoambukiza (NCD) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Ukiwa na sonona baadhi ya dalili zinazoweza kukupata ni kukosa hamu ya kula pia kukosa hamu ya tendo la ndoa,” amesema Dkt Lema.

Dalili nyingine alizitaja kuwa ni hali ya kutotaka kujumuika, kuhisi uchovu, kukosa usingizi na kushindwa kutekeleza majukumu ya kawaida ya kila siku.

Amezitaja dalili nyingine kuwa ni huzuni endelevu, kusahau, ugumu wa maamuzi, kukosa umakini, kujihisi kuwa na hatia kwa mambo yasiyokuhusu na maumivu ya mwili yasiyoweza kubainika kwa vipimo hospitalini.

Inapotokea mtu kujihisi kuwa na dalili hizo, Dkt Lema alishauri kuwahi hospitali na kuonana na mtaalamu wa magonjwa ya akili ili kupata msaada.

Ili kuepuka sonona, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasoambukiza (TANCDA), Profesa Andrew Swai alisema ni kuzungumza na watu wa karibu unaowaamini juu ya matatizo yanayokukabili.

Alisema wakati mwingine sonona inasababishwa na mambo ya kutetwa na watu wengine lakini akasema anachoweza kufanya mtu ni kutojali kwa sababu mwishowe watachoka na hawatakudhuru kwa lolote.

“Kumbuka ule wimbo unaosema ‘Waache waseme, mwisho watachoka,” ameonya Profesa Swai.

Hatua nyingi amesema ni mtu kukubali matatizo ya dunia na kuyakabili kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamaoja na kuomba ushauri.

Ameonya kuhusu kuwa na tama hasa kwa mambo ambayo yako nje ya uwezo kama vile kama mwenzako kajenga ghorofa na wewe kutaka kufanya hivyo wakati uwezo huna.

Ameonya kuwa sonona ni miongoni mwa magonjwa yanayowasumbua wengi na yanaweza kuwa chanzo au kuhatarisha zaidi hali ya kiafya kwa wanaougua NCD.

Ametaja miongoni mwa NCD kuwa ni kisukari, shinikizo la damu, saratani, siko seli, pumu na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa.