October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ruvuma yatoa vitambulisho vya wajasiriamali zaidi ya 72,000

Na Albano Midelo, TimesMajira Online, Ruvuma

MKOA wa Ruvuma umefanikiwa kutoa vitambulisho kwa wajasirimali wadogo 59,279 mwaka 2019 na vitambulisho 13,827 vimetolewa kwa wajasirimali wadogo hadi kufikia Oktoba 23, mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akifungua Baraza Maalum la Biashara Mkoa wa Ruvuma kwenye ukumbi wa hoteli ya Herritage Colttage mjini Songea

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme wakati anafungua mkutano wa Baraza Maalum la Biashara la Mkoa wa Ruvuma kwenye ukumbi wa Herritage Cottage mjini Songea.

Amesema mkoa umejikita kuhakikisha kuwa malengo ya serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda yanafanikiwa ambapo hadi kufikia Juni 2020 Mkoa wa Ruvuma ulikuwa na jumla ya viwanda 3,485.

Kwa mujibu wa Mndeme kati ya viwanda hivyo,viwanda vikubwa sita,viwanda vya kati 25,viwanda vidogo 190 na viwanda vidogo sana 3,264 na kwamba utekelezaji huo unaendelea kufanywa na sekta binafsi na sekta ya umma.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Masoko Songea Leonard Chinga akitoa ushuhuda walivyonufaika na vitambulisho.

“Ili kukuza sekta ya Viwanda,Mkoa wa Ruvuma umeendelea kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo,ambapo Julai 25,2020 mkoa uliandaa maonesho ya viwanda na uwekezaji kwa lengo la kutangaza fursa zilizopo’’,amesema Mndeme.

Amesema katika kongamano hilo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizindua Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa na kwamba Mwongozo huo umesambazwa kwenye Taasisi mbalimbali ambapo hadi sasa wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza ni 22.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC) Emanuel Alphance amelitaja lengo la kufanyika Baraza hilo la biashara ni kufanya tathmini ya mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kuangalia mikakati na vipaumbele kwa upande wa sekta binafsi na umma katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mwakilishi huyo wa TNBC amesema mfumo huo wa majadiliano kupitia mabaraza ya Taifa,mikoa na wilaya,unatokana na serikali kuwezesha sekta zote kushiriki katika mipango ya serikali,sanjari na uwepo wa mazingira bora ya kufanya biashara.

Amesema Mabaraza ya biashara yameanzishwa rasmi kwa waraka namba moja wa Rais wa mwaka 2001 na kufuatiwa na azimio la kuanzisha mabaraza ya biashara ya mikoa na wilaya kati ya mwaka 2005 hadi 2008.

Kwa upande wake Yohana Nchimbi ambaye ni Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Ruvuma,amesema TCCIA kama sekta binfasi imenufaika kuanzia wafanyabiashara wa ngazi ya chini hadi juu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ya serikali ya Awamu ya Tano.

“Kwa jitihada kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano,hatuna sababu ya kutokutambua mafanikio haya,hatuwezi kufumba macho tukasema eti hatuyaoni, hatuyasikii, hatunufaiki nayo,wafanyabiashara walioshiriki katika Baraza hilo watakuwa mashahidi wakubwa walionufaika’’ amesisitiza Nchimbi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Masoko Songea(UWABIMASO) amempongeza Rais Magufuli kwa kuwawezesha wajasiriamali wadogo vitambulisho ambavyo vimeondoa usumbufu mkubwa waliokuwa wanakabiliwa nao.

Amesema kwa mwaka wafanyabiashara wadogo walikuwa wanalipa ushuru wa zaidi ya shilingi 150,000 ambapo hivi sasa baada ya kupata vitambulisho kwa shilingi 20,000, wafanyabiashara wameweza kutunza fedha zao na kufanya biashara bila usumbufu wowote.