November 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Tanga yarudisha Sh. milioni 151.3

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Tanga

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga imefanikiwa kuirejeshea Serikali zaidi ya sh.milioni 151.3,katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, kupitia ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato, matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo, uchambuzi wa mifumo pamoja na hatua mbalimbali za kisheria.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, kuimarisha uwajibikaji kwa watendaji wa umma na kudhibiti mianya inayoweza kusababisha upotevu wa mapato ya serikali.

Akitoa taarifa ya utendaji wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga kwa kipindi hicho kwa waandishi wa habari jijini humo kwa niaba ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Mariam Mayaya amesema, taasisi hiyo imeendelea kufanya ufuatiliaji wa kina katika maeneo mbalimbali yenye viashiria vya ubadhirifu, uzembe na mianya ya upotevu wa fedha za umma.

Mayaya amesema,katika kipindi hicho, TAKUKURU ilifuatilia matumizi ya sh.milioni 57.3 zilizotumika katika utekelezaji wa miradi 99 ya maendeleo iliyokuwa katika sekta za maji, afya, elimu na miundombinu, ambapo kasoro mbalimbali zilizobainika zilifanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi.

Amesema,ufuatiliaji huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazostahili kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali, huku akisisitiza kuwa taasisi hiyo haitasita kuchukua hatua pale inapobaini viashiria vya matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma.

Katika sekta ya elimu, TAKUKURU ilifanya ufuatiliaji wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Stahabu uliokuwa na thamani ya sh.milioni 984.2 ambapo ilibaini kasoro katika vifaa vya ujenzi vilivyotumika.

Kasoro hiyo ilihusisha milango na fremu 27 zenye thamani ya sh.milioni 10.665,zilizokuwa zimefungwa katika mradi huo, ambazo hazikuwa na ubora unaotakiwa kwa mujibu wa maelekezo yaliyopo kwenye Bill of Quantities (BOQ), inayobainisha mahitaji na viwango vya vifaa vinavyotakiwa katika mradi wa ujenzi.

Baada ya kubaini kasoro hizo, TAKUKURU ilishauri milango na fremu hizo kuondolewa na kuwekwa nyingine zenye ubora unaokidhi viwango vilivyoainishwa katika BOQ, hatua ambayo ilitekelezwa na kuhakikisha mradi unazingatia ubora uliokusudiwa.

Amesema hatua hiyo inaonesha umuhimu wa ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, kwani bila usimamizi madhubuti, wananchi wanaweza kupewa huduma zisizokidhi viwango licha ya Serikali kutumia fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika eneo la uchambuzi wa mifumo, TAKUKURU Mkoa wa Tanga ilifanya uchambuzi wa mfumo wa usimamizi wa mapato na matumizi katika Vyombo vya Watumiaji Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO), ambapo ilibaini uwepo wa madeni ya muda mrefu yaliyokuwa yakidaiwa na vyombo hivyo kutoka kwa watumiaji wa huduma za maji, wakiwemo baadhi ya taasisi za serikali.

Amesema baada ya kubaini changamoto hiyo, TAKUKURU iliandaa warsha iliyowakutanisha wadau husika kwa lengo la kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto za madeni pamoja na kuimarisha usimamizi wa mapato katika vyombo hivyo.

Kupitia hatua hiyo, jumla ya sh.milioni  21.654, zilirejeshwa katika Wilaya ya Lushoto, huku Wilaya ya Kilindi ikirejeshewa sh.milioni 12.516 fedha ambazo zilikuwa zinadaiwa na vyombo vya watumiaji maji.

Hata hivyo TAKUKURU Mkoa wa Tanga ilifuatilia matumizi ya mashine za kielektroniki za ukusanyaji mapato (POS) zinazotumiwa na halmashauri, ambapo ilibaini kuwepo kwa wadaiwa mbalimbali ambao hawakuwa wametekeleza wajibu wao wa kuwasilisha mapato stahiki kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi.

Ufuatiliaji huo ulibaini kuwa jumla ya sh.milioni  47.020,zilikuwa hazijawasilishwa kwa halmashauri, hali iliyokuwa ikihatarisha upatikanaji wa mapato ya serikali na kuweza kuathiri utekelezaji wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.Ambapo TAKUKURU ilichukua hatua za kudhibiti hali hiyo na kuhakikisha fedha hizo zimerejeshwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi na hivyo kuzuia fedha hizo kupotea.