November 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Elimisha yawajengea uwezo watetezi haki za wanawake/ wasichana

Na Mwandishi wetu, TimesmajiraOnline, Kyela

SHIRIKA lisilo la kiserikali la ELIMISHA linalojihusisha na masuala ya wanawake, vijana na watoto limeanza kutekeleza mikakati ya kuwaimarisha watetezi wa haki za wanawake na wasichana kwa kuwapatia mafunzo yatakayowawezesha kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Debora Mwanyanje, amesema tafiti zinaonesha kuwa wanawake na wasichana ni miongoni mwa makundi yanayoathiriwa zaidi na vitendo vya ukatili wa kijinsia, hali inayohitaji kuwepo kwa juhudi za pamoja katika kuwalinda na kutetea haki zao.

Mwanyanje ameyasema hayo Novemba 25, 2026, wakati wa mafunzo kwa watetezi wa haki za wanawake na wasichana yaliyofanyika wilayani Kyela, mkoani Mbeya, yenye lengo la kujenga uwezo na kuweka mikakati ya pamoja ya kusaidia makundi hayo.

Amesema wanawake na wasichana wanahitaji kupewa kipaumbele katika juhudi za kupinga ukatili wa kijinsia kutokana na changamoto wanazokutana nazo, huku akieleza kuwa mara nyingi wanawake huwa sehemu muhimu ya kwanza ya msaada kwa watoto wa kike wanapokumbana na changamoto.

“Tunatetea jamii nzima, lakini wanawake na wasichana ni miongoni mwa makundi yanayohitaji nguvu zaidi ya utetezi kutokana na changamoto za ukatili wa kijinsia zinazowakabili,” amesema Mwanyanje.

Ameeleza kuwa lengo la kukutana na mashirika pamoja na watetezi wa haki za wanawake na wasichana wilayani Kyela ni kuunganisha nguvu na kujenga ushirikiano kati ya taasisi zenye malengo yanayofanana ili kuongeza ufanisi wa shughuli za utetezi.

Amesema shirika hilo limeanza mpango huo kwa kutoa mafunzo katika Jiji la Mbeya, Kyela na Rungwe, kwa lengo la kuunganisha nguvu za watetezi na mashirika mbalimbali katika ngazi ya mkoa mzima.

“Unapofanya shughuli za utetezi, ni muhimu kuungana na mashirika mengine yenye mwelekeo unaofanana ili kupata matokeo chanya zaidi kuliko kufanya kazi kama shirika moja pekee. Ndiyo maana tumeanza kuunganisha nguvu kupitia mafunzo haya,” amesema.

Kwa upande wake, Fred Mwangomba, ambaye ni mtoa elimu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia, amesema watoto wa kike wanahitaji kupewa elimu na ulinzi zaidi ili waweze kutambua na kuepuka mazingira yanayoweza kuwaweka katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili.

Amesema elimu kwa watoto, familia na jamii kwa ujumla ni muhimu katika kuimarisha uelewa kuhusu haki za watoto na kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Naye Joyce Fred amesema mafunzo waliyopata yatawaongezea uwezo wa kutetea haki za wanawake na wasichana, ambao wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali za ukatili wa kijinsia.

Ameongeza kuwa watatumia ujuzi walioupata kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha ushiriki wa wadau mbalimbali katika kupinga ukatili huo.