November 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ETDCO yaimarisha upatikanaji umeme mgodi wa GGM

Na Mwandishi wetu,TimesMajira

KAMPUNI ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme(ETDCO), kwa niaba ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), imefanikiwa kujenga njia mbili za kusafirisha umeme wa kilovolti 33 zenye urefu wa kilomita sita kutoka Kituo cha Mpomvu hadi Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM),hatua iliyowezesha mgodi huo kuunganishwa na Gridi ya Taifa.

Utekelezaji wa mradi huo umewezesha kupunguza matumizi ya majenereta yanayotumia mafuta ya dizeli na uzalishaji wa hewa ukaa kwa takribani tani 50,000 kwa mwaka, huku ukiimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea ufanisi wa shughuli za uchimbaji wa dhahabu.

Akizungumzia juzi mkoani humo, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Geita,Mhandisi Jahulula Jahulula amesema kuunganishwa umeme huo na Gridi ya Taifa kumesaidia kupunguza gharama za uzalishaji,ambazo awali zilikuwa kubwa kutokana na utegemezi wa majenereta ya dizeli.

Amesema gharama za kuzalisha umeme kwa kutumia majenereta hayo zilikuwa zaidi ya mara mbili hadi tatu ikilinganishwa na gharama za kutumia umeme.

Ameeleza kuwa mgodi huo kwa sasa unatumia takribani megawati 36 za umeme kutoka TANESCO, hali inayosaidia kuongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji na kupunguza gharama za uendeshaji.

Kwa upande wake Mhandisi wa Umeme kutoka GGM,Abraham Zoa ameipongeza ETDCO kwa kushirikiana na TANESCO kutekeleza mradi huo,huku akisema uwekezaji huo umeleta manufaa makubwa kwa mgodi na kuendelea kusaidia uzalishaji wa dhahabu kwa gharama nafuu.

“Mradi huu umeonesha umuhimu wa uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya umeme, hususan kwa kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wawekezaji na viwanda,”amesema

Aidha ameipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika nchini, ni hatua muhimu katika kuvutia uwekezaji na kukuza shughuli za kiuchumi,”amesema