November 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rufaa Mbeya, Madaktari Bingwa Uingereza Kwenye Diplomasia ya Tiba

Na Mwandishi, TimesmajiraOnline, Mbeya

HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imeendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Uingereza katika sekta ya afya kupitia ushirikiano na taasisi ya madaktari bingwa ya BAUS Urolink, unaolenga kuboresha huduma za kibingwa, kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani na kubadilishana uzoefu.

Hatua hiyo imebainika Novemba 16, 2026, jijini Mbeya, wakati Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt. Godlove Mbwanji, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa madaktari bingwa kutoka taasisi ya BAUS Urolink ya Uingereza, sambamba na kuanza kwa kambi maalumu ya matibabu na mafunzo ya magonjwa ya mfumo wa mkojo (Urology).

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Mbwanji amesema ushirikiano huo wa kimataifa ni sehemu ya matokeo ya diplomasia ya Tanzania inayowezesha wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kuja kushirikiana na madaktari wazawa, hususan katika maeneo ya Mbeya, Katavi na mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini.

“Tunawashukuru na kuwapongeza kwa ushirikiano huu wenye tija. Niwasihi muendelee kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu ya Tanzania na hospitali yetu mnaporejea nchini kwenu au mnapotembelea mataifa mengine,” amesema Dkt. Mbwanji.

Kwa upande wake, Kiongozi wa ujumbe wa Urolink, Dkt. Suzie Venn, aliyeambatana na madaktari bingwa wenzake, Dkt. Paul Anderson na Dkt. Stephen Griffin, ameushukuru uongozi wa hospitali hiyo kwa mapokezi mazuri, akisema hatua hiyo inaakisi uhusiano mzuri na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Uingereza.

Dkt. Venn pia amepongeza maboresho yaliyofanyika katika miundombinu na upatikanaji wa vifaa tiba hospitalini hapo, huku akieleza dhamira ya taasisi yake kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu unaohusisha kubadilishana uzoefu, kuwajengea uwezo madaktari wazawa na kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa wa watu wazima na watoto.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuendelea kuwa fursa muhimu katika kuimarisha huduma za matibabu ya mfumo wa mkojo, kuongeza ujuzi wa wataalamu wa ndani na kupanua upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi wa Nyanda za Juu Kusini.