November 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mwigulu ataka ushirikiano viongozi wa MSM

Na Yusuph Musa,TimesMajira Online, Mwanza

WAZIRI Mkuu wa Tanzania Dkt Mwigulu Nchemba ametaka kuwe na ushirikiano kwa viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM) katika kuwatumikia wananchi, kwani mivutano itafanya kuchelewesha shughuli za maendeleo za wananchi.

Ameyasema hayo Novemba 16,2026 wakati anafungua Mkutano Mkuu wa 40 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika jijini Mwanza.

Dkt. Mwigulu amesema kumekuwa na mivutano miongoni mwa mameya, wenyeviti, wakurugenzi na wakuu wa wilaya, jambo ambalo halina tija, hivyo kutaka kujenga ushirikiano kwa kufanya kazi za wananchi.

“Mnatakiwa kufanya kazi kwa ushitikiano na kuondoa mivutano. Hatutaki mfanye urafiki kati ya Mwenyekiti na Mkurugenzi, bali ushirikiano. Hivyo tuondoe migongano kati ya mameya na wakurugenzi, na wenyeviti, wakurugenzi na wakuu wa wilaya”amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema kuhusu madiwani kuongezewa posho, ametaka wavute subira, huku suala lao likiendelea kuchakatwa, na kuongeza kuwa Serikali imekuwa ikikamilisha miradi ya kimkakati kama vile Bwawa la Mwalimu Nyerere, Reli ya Kisasa ya SGR, na Daraja la Kigongo- Busisi, wakati huo huo wakikabiliwa na ongezeko la ujenzi wa vyumba vya madarasa mwaka 2028.

Naibu Waziri wa TAMISEMI Dkt.Festo Dugange amewataka Wajumbe wa ALAT Taifa kutoka na maazimio yenye tija ambayo yatatekekezeka kwa ajili ya kusaidia kusukuma mbele miradi ya wananchi

Awali, Mwenyekiti wa ALAT Taifa Sima Sima, pamoja na mambo mengine, ameiomba Serikali kuwaongezea posho madiwani sababu wao wapo karibu na wananchi, pia posho hiyo kwa sasa imekuwa ni ndogo, na haikidhi mahitaji ya sasa