November 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Dugange atoa maelekezo sita kwa halmashauri nchini

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza

NAIBU Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, ametoa maelekezo sita kwa viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa hapa nchini huku akiwataka kuyatekeleza kwa vitendo ili kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Dkt. Dugange ametoa maelekezo hayo Novemba 16, 2026, wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 40 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), uliofanyika jijini Mwanza na kufunguliwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Katika maelekezo hayo, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha utawala bora na uwajibikaji katika halmashauri ambapo viongozi wanapaswa kusimamia rasilimali za umma kwa uwazi na kuhakikisha zinatumika kwa manufaa ya wananchi.

Pia, amewataka viongozi kuhakikisha maazimio ya mikutano yanatekelezwa badala ya kubaki kwenye maandishi, huku akisisitiza halmashauri kuongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia matumizi ya fedha kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo.

Aidha, amesisitiza usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati, kuzingatia viwango vya ubora na kutoa thamani ya fedha zinazotumika.

Sanjari na hayo amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa kuimarisha huduma za msingi zikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa viongozi wa ALAT na halmashauri zote hapa nchini, huku mipango ya maendeleo ikiendana na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema utekelezaji wa maelekezo hayo ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa Serikali za Mitaa na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazochochea maendeleo katika maeneo yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa ALAT Taifa Sima Constantine,ameiomba Serikali kuwaongezea posho madiwani sababu wao wapo karibu na wananchi,kwani imekuwa ndogo na haikidhi mahitaji ya sasa.

“Kwa miaka 12, miaka 13 tumekuwa mashuhuda gharama za maisha zimebadilika kwa kiasi kikubwa,mara ya mwisho diwani anaongezewa posho yake mkate ulikuwa unauzwa sh.500,”amesema.