November 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watakwimu watakiwa kujiandaa mapinduzi ya teknolojia

Na Joyce Kasiki,Dodoma


WATAALAM wa Takwimu nchini wametakiwa kuongeza maarifa na umahiri katika matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Unde (AI), Big Data na Data Science ili kukabiliana na mabadiliko ya taaluma hiyo na mahitaji yanayoongezeka katika soko la ajira.


Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uratibu, Utafiti na Shughuli za Kitakwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), James Mbongo, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama cha Wataalamu wa Takwimu Tanzania (TASTA) uliofanyika jijini Dodoma.


Mbongo amesema mabadiliko ya teknolojia yamebadili namna taarifa zinavyokusanywa, kuchambuliwa na kutumika, hivyo wataalamu wa takwimu wanapaswa kujifunza mbinu mpya zitakazowawezesha kutoa taarifa sahihi na zenye tija kwa maendeleo ya nchi.


Amesema takwimu zina nafasi kubwa katika kuongoza maamuzi ya Serikali na sekta binafsi, kuanzia hatua za kupanga mipango, utekelezaji wake hadi kupima mafanikio yaliyopatikana.


Ameeleza kuwa maendeleo ya taaluma hiyo hayawezi kutegemea uwepo wa taasisi na vyama pekee, bali yanahitaji uwekezaji wa kutosha katika kuwajengea uwezo wataalamu, kuongeza nafasi zao katika taasisi mbalimbali na kuitambua thamani ya mchango wao.


Amebainisha kuwa wataalamu hao wanapaswa kutumia maarifa yao kutoa uchambuzi unaoonesha mahitaji halisi ya uwekezaji na matokeo yanayoweza kupatikana katika sekta mbalimbali.


Akifafanua umuhimu huo, ametumia mfano wa sekta ya kilimo, akisema mtaalamu wa takwimu anapaswa kuwa na uwezo wa kutathmini kiasi cha uwekezaji kinachohitajika, makadirio ya uzalishaji na matokeo yanayotarajiwa katika kipindi cha miaka mitano.


Kuhusu maandalizi ya kitaaluma, Mbongo amesema mafunzo mafupi kuhusu teknolojia mpya hayatoshi kuwapa wataalamu uwezo unaohitajika, akisisitiza umuhimu wa kujifunza kwa kuendelea na kutumia fursa za mafunzo zinazopatikana kupitia majukwaa mbalimbali ya mtandaoni.


Amesema ujuzi wa Big Data na Data Science unazidi kuwa hitaji muhimu katika ulimwengu wa ajira, hivyo wataalamu wanapaswa kujijengea uwezo wa kushindana na kukidhi mahitaji ya soko la sasa na baadaye, hasa kuelekea mwaka 2030.

Mwenyekiti wa TASTA, Abdallah Mhagama


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TASTA, Abdallah Mhagama, amesema chama hicho kimejikita katika kuwakutanisha wataalamu wa takwimu kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kuimarisha ushirikiano na kuongeza ubora wa takwimu zinazozalishwa nchini.


Mhagama amesema ingawa NBS ndiyo taasisi kuu yenye jukumu la kuratibu na kuzalisha takwimu rasmi, taasisi nyingine pia zinashiriki katika uzalishaji wa taarifa kupitia Mfumo wa Taifa wa Takwimu, jambo linalohitaji uratibu na matumizi ya viwango vinavyofanana.


Amesema ushirikiano kati ya wazalishaji wa takwimu ni muhimu katika kuhakikisha taarifa zinazotolewa zinaaminika na zinakidhi viwango vya kitaifa.


Ameongeza kuwa TASTA imeweka mkazo katika kuwajengea uwezo wanachama wake, hususan vijana, kwa kuwaandaa kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji mapya ya taaluma ya takwimu.


Kwa mujibu wa Mhagama, chama hicho kimekuwa kikiandaa mafunzo yanayohusu matumizi ya teknolojia katika uchambuzi wa taarifa, yakiwemo matumizi ya Big Data na Akili Unde, ili kuongeza ufanisi na uwezo wa kitaaluma kwa wanachama.


Amesema TASTA pia inashirikiana na Serikali kuhakikisha takwimu zinazozalishwa zinawafikia walengwa na kutumika katika kufanya maamuzi, badala ya kuhifadhiwa bila kuwa na matumizi yenye tija.


Amefafanua kuwa katika kutekeleza jukumu hilo, chama hicho kimekuwa kikishirikiana na NBS kufanya uchambuzi na kutoa elimu kuhusu baadhi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ili wananchi waelewe namna takwimu zinavyoweza kusaidia katika kupanga shughuli za maendeleo.


Katika eneo la ushirikiano, Mhagama amezitaja Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Afrika (UNECA), NBS, Ofisi ya Takwimu ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na taasisi nyingine za Serikali na mashirika mbalimbali kuwa miongoni mwa wadau wanaoshirikiana na chama hicho.


Amesema kuongezeka kwa wanachama wawili kutoka Zanzibar mwaka huu ni hatua inayopanua wigo wa ushiriki na kuimarisha uwakilishi wa wataalamu wa takwimu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.


Ameeleza kuwa mkutano mkuu wa mwaka huu pia unalenga kutathmini utekelezaji wa shughuli za mwaka uliopita, kujadili mafanikio na changamoto zilizojitokeza, kupitia mipango na bajeti ya kipindi kijacho pamoja na kutambua wanachama walioonesha mchango mkubwa katika taaluma hiyo.


Aidha, amesema mkutano huo utatumika kuchagua viongozi wapya watakaosimamia chama kwa kipindi kijacho, ambapo nafasi zitakazoshindaniwa ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu mkuu na mweka hazina.

Makamu Mwenyekiti wa TASTA, Mariamu Kinabo


Naye Makamu Mwenyekiti wa TASTA, Mariamu Kinabo, amesema upungufu wa rasilimali fedha ni miongoni mwa changamoto zinazokwamisha chama kuwafikia na kuwaunganisha wanachama waliopo katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini.


Amesema umbali wa maeneo wanakoishi wanachama unasababisha gharama kubwa za usafiri, malazi, chakula na maandalizi ya mikutano, hali inayopunguza uwezo wa chama kuwakutanisha wataalamu wote kwa wakati mmoja.


Kinabo amesema licha ya kuwepo kwa mpango wa kufanya mikutano mara kadhaa kwa mwaka, changamoto za kifedha zimekuwa zikifanya mikutano hiyo kufanyika kwa wastani wa mara moja kwa mwaka.


Ameeleza kuwa hali hiyo inahitaji chama kuboresha usimamizi wa fedha na kutumia rasilimali zilizopo kwa uangalifu ili kuhakikisha shughuli zilizopangwa zinatekelezwa na wanachama wa maeneo yote wanapata fursa ya kushiriki.


Amesema mikutano mikuu ni sehemu muhimu ya uwajibikaji wa chama kwa kuwa wanachama hupata nafasi ya kupitia utekelezaji wa shughuli zilizopita, kujadili mipango na bajeti mpya pamoja na kuchagua viongozi watakaohudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.


Pamoja na changamoto hizo, Kinabo amesema TASTA itaendelea kutafuta njia za kuimarisha ushiriki wa wanachama na kuongeza ufanisi wa shughuli zake kwa lengo la kukuza na kuendeleza taaluma ya takwimu nchini.