Na Joyce Kasiki, Dodoma
SPIKA wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu, ameitaka Serikali, sekta binafsi na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhakikisha bunifu zinazofanywa na vijana nchini zinafikia sokoni na kuanza kutumika katika jamii.
Amesema bunifu hizo hazipaswi kubaki katika maonesho na majaribio pekee, bali zinapaswa kupewa fursa ya kuzalishwa na kuuzwa ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi na kukuza uchumi.
Zungu ametoa agizo hilo Novemba 4, 2026, alipotembelea Maonesho ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yanayoendelea nje ya viwanja vya Bunge.
Miongoni mwa bunifu alizoziona ni mkanda maalumu unaotumika hospitalini kusaidia kudhibiti upotevu mkubwa wa damu kwa wanawake wakati wa kujifungua na hivyo kuokoa maisha, gesi ya kupikia inayotokana na maji pamoja na kemikali inayotumika kulainisha bidhaa za ngozi viwandani.
Akizungumza kuhusu bunifu hizo, Zungu amesema pamoja na ubora wake, jambo muhimu ni kuhakikisha kuna mipango madhubuti ya kuzipeleka sokoni.
Amesisitiza umuhimu wa kubaini taasisi zitakazonunua bidhaa hizo, masoko yatakayozihitaji na namna Serikali pamoja na sekta binafsi zitakavyoshirikiana kuwawezesha vijana kuzalisha na kuuza bunifu zao.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali ina matumaini makubwa na uwezo wa vijana katika nyanja za sayansi na teknolojia.
Amesema kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Mfuko wa Ubunifu wa Samia (Samia Innovation Fund), Serikali inaendelea kuwaunga mkono wabunifu ili bidhaa zao ziweze kuendelezwa na kufikia hatua ya kuingia sokoni.
Aidha, amesema uwekezaji katika elimu ya sayansi, ufadhili wa masomo na tafiti ni sehemu ya juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.

More Stories
Magesa awataka watendaji kufuata sheria ukusanyaji wa mapato
Chalamila kwenda Qatar kuishangilia Serengeti Boys
Rc.Chalamila atangaza rasmi mikakati ya kuboresha Dar