Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
TANZANIA imeendelea kushiriki mijadala mbalimbali inayolenga kuendeleza matumizi ya nishati ya jua duniani katika Mkutano Mkuu wa Tisa wa Muungano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (ISA) unaofanyika New Delhi, India, sambamba na kufanya mazungumzo na kampuni mbalimbali za kimataifa zinazojishughulisha na teknolojia ya nishati hiyo.
Mazungumzo na kampuni hizo za nishati jua yamefanyika tarehe 4 Novemba 2026, pembezoni mwa mkutano huo, yakiongozwa na Bw. Emilian Nyanda kutoka Wizara ya Nishati, ambaye pia ni Mwakilishi wa Tanzania katika ISA lengo likiwa ni kutafuta wawekezaji watakaoshirikiana na Serikali katika kupanua huduma ya umeme hususan maeneo ambayo bado hayajafikiwa na Gridi ya Taifa
Katika mazungumzo hayo,Nyanda amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji katika nishati jadidifu, hususan umeme wa jua, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika, ikiwemo katika maeneo ya visiwa na maeneo mengine ambayo bado hayajafikiwa na Gridi ya Taifa, sambamba na kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Pembezoni mwa mkutano wa ISA,Nyanda amekutana na watendaji wa kampuni ya Shakti Pumps, wakiongozwa na Mtendaji Mkuu,Ramesh Patidar, ambaye ameeleza kuwa kampuni hiyo inajishughulisha na teknolojia ya pampu za maji zinazotumia nishati ya jua kwa ajili ya kusambaza maji katika jamii na kuendesha miradi ya umwagiliaji ambayo ni muhimu katika kuongeza tija ya kilimo na kuboresha upatikanaji wa maji, hususan maeneo ya vijijini.
Aidha, Nyanda amefanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Enerzy AI, Mazhar Hussein, inayojishughulisha na mifumo ya kidijitali ya kusimamia na kudhibiti mitambo ya umeme wa jua. Mifumo hiyo ina uwezo wa kufuatilia utendaji wa mitambo, kubaini hitilafu na kutabiri mwenendo wa uzalishaji wa umeme kwa kuzingatia hali ya mionzi ya jua.

Katika hatua nyingine, amekutana na Mkuu wa Sehemu ya Biashara wa Kampuni ya Ecozen, Kishan Dhameliya, ambapo wamejadili matumizi ya nishati ya jua katika miradi ya umwagiliaji na mifumo ya kuhifadhi mazao kwa kutumia vyumba vya baridi vinavyoendeshwa kwa umeme wa jua.
Kampuni ya Ecozen tayari inatekeleza shughuli zake nchini Tanzania, ikiwemo ufungaji wa mifumo ya umwagiliaji inayotumia nishati ya jua katika mikoa ya Dodoma na Arusha.

Kampuni hiyo pia inatoa teknolojia ya vyumba vya baridi vinavyowezesha wakulima, wafugaji na wafanyabiashara kuhifadhi mazao yao kwa muda mrefu zaidi, hivyo kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuongeza fursa za masoko.
Katika mazungumzo yake na kampuni hizo, Nyanda amesisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuwakaribisha wawekezaji wenye teknolojia na uzoefu katika uzalishaji na matumizi ya nishati ya jua ili kushirikiana na Serikali katika kupanua huduma za umeme, kuongeza matumizi ya teknolojia safi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.


More Stories
Dkt.Mabula ataka kasi mpya maendeleo Tabora
Wananchi wahamasishwa kujiunga na bima ya afya
Rais Samia apiga kura Chamwino,kumpata Mrithi wa Ndejembi