November 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

THTUB kuimarisha usimamizi wa haki,utawala bora


Na Joyce Kasiki Dodoma


MWENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Wakili Dunford Mpelumbe, amesema Tume hiyo imejipanga kuimarisha usimamizi na ulinzi wa haki za binadamu nchini kwa kuhakikisha malalamiko ya wananchi yanapokelewa, kuchunguzwa na kushughulikiwa bila upendeleo.


Mpelumbe ameyasema hayo leo Nov 2,2026 baada ya kuapishwa na kupokelewa rasmi na watumishi wa tume hiyo, ambapo amebainisha kuwa wamejipanga kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maelekezo, vipaumbele na changamoto zinazoikabili sekta ya haki za binadamu.


Amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, Tume itaendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha mifumo ya kisheria, kisera na kitaasisi ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao za msingi za kiraia na kijamii, ikiwemo upatikanaji wa huduma bora za afya na maji safi na salama.


Aidha, amesema Tume itaongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora, sambamba na kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imesaini na kuridhia.


Amesisitiza kuwa katika kutekeleza majukumu hayo, tume itazingatia weledi, uadilifu, uwajibikaji na kutenda haki bila upendeleo, kwa lengo la kuhakikisha misingi ya haki za binadamu na utawala bora inazingatiwa nchini.
Imeandaliwa na Merina Makasi