November 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SGA yaimarisha utoaji huduma bora kwa wateja

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online

KAMPUNI ya SGA Security imeendelea kuimarisha dhamira yake ya kutoa huduma bora kwa wateja na kuchangia ustawi wa jamii kupitia mfululizo wa shughuli zilizofanyika Oktoba.

Shughuli hizo ziliunganisha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, kampeni ya Pink October na mipango mbalimbali ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika matawi yake nchini Tanzania.

Katika kampeni ya afya, SGA Security ilishirikiana na taasisi za afya katika mikoa mitano kuwezesha huduma za uchunguzi wa afya bila malipo kwa wananchi. Kampeni hiyo ilianza Oktoba 9 jijini Dar-es-Salaam katika eneo la Tanganyika Packers, karibu na Soko la Kawe, kwa ushirikiano na Zahanati ya Kawe.

Zoezi hilo liliendelea katika maeneo ya Stendi ya Kabwe mkoani Mbeya, Mnada Mpya mkoani Dodoma, Soko la Tengeru mkoani Arusha na Soko la Samaki mkoani Mwanza, kupitia ushirikiano na Hospitali ya Meta, Hospitali ya Dodoma General, Hospitali ya Levolosi na Hospitali ya Bugando, mtawalia.

Shughuli hizo ziliwapatia wananchi fursa ya kupata huduma za uchunguzi wa afya huku zikihamasisha umuhimu wa kujikinga na magonjwa na kufuatilia afya zao mara kwa mara.

Mbali na huduma za uchunguzi wa afya, SGA Security pia iliunga mkono zoezi la uchangiaji damu katika maeneo yote matano yaliyofikiwa na shughuli za CSR.

Zoezi hilo lililenga kusaidia kupunguza uhaba wa damu katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu kwa sababu mbalimbali za kiafya, wakiwemo wanaopata matibabu ya saratani na wanawake wanaohitaji damu wakati wa kujifungua. Mpango huo ulisisitiza umuhimu wa uchangiaji damu wa hiari katika kuokoa maisha.

Sambamba na shughuli hizo za afya, SGA Security iliadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kutembelea baadhi ya wateja wake muhimu katika ofisi zao ili kuwashukuru kwa kuendelea kuiamini kampuni na kudumisha ushirikiano. Ziara hizo zilihusisha hafla fupi za kukata keki na mazungumzo ya ana kwa ana, yaliyolenga kuimarisha uhusiano na wateja pamoja na kutambua mchango wao katika ukuaji endelevu wa kampuni.

Akizungumzia mipango hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Security, Jonathan Geleta amesema,kuwa kuridhika kwa wateja na ustawi wa jamii ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vya kampuni.

“Wateja wetu ni sehemu muhimu ya mafanikio yetu, na ustawi wa jamii tunazozihudumia unaendelea kuwa kipaumbele. Kupitia mipango hii, tunaimarisha uhusiano wetu na wateja huku tukichangia afya na ustawi wa jamii katika maeneo mbalimbali nchini,”amesema Geleta.

Ikiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 42 nchini Tanzania, SGA Security hutoa huduma mbalimbali za kiusalama, zikiwemo ulinzi, usafirishaji wa fedha na vitu vya thamani, huduma za kukabiliana na dharura pamoja na mifumo ya kisasa ya usalama wa kielektroniki. Kampuni ina mtandao wa matawi katika maeneo mbalimbali nchini na inaajiri maelfu ya wataalamu, huku huduma zake zikiungwa mkono na vyeti vya viwango vya kimataifa vya ISO.

Kupitia shughuli zake za mwezi Oktoba, SGA Security inaendelea kuonesha namna ambavyo kuthamini wateja, kushirikiana na wadau pamoja na kutekeleza wajibu wa kampuni kwa jamii vinavyoweza kwenda sambamba na dhamira yake kuu ya kutoa huduma za kiusalama nchini Tanzania.