Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MIXX Tanzania, inapanga kupanua huduma zinazopatikana kupitia mtandao wake wa mawakala zaidi ya 270,000 nchini, ili kuwaongezea fursa za kipato nje ya kamisheni wanazopata kutokana na miamala ya kuweka na kutoa fedha.
Mipango hiyo ni sehemu ya dhamira ya kampuni kuimarisha ushirikiano na mawakala wake kwa kupanua fursa za biashara, kuimarisha mawasiliano na kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali katika shughuli zao za kila siku.
Akizungumza katika hafla ya ‘Mixx Wakala Brunch’ iliyofanyika Dar es Salaam hivi karibuni, iliyoadhimisha miaka 16 ya ushirikiano na mawakala, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx Tanzania, Louis-Olivier Favot, amesema mtandao huo sasa unawahudumia Watanzania takribani milioni 28.
“Tangu enzi za Tigo Pesa hadi leo Mixx, ninyi ndio mmetusaidia kujenga biashara hii. Mnafungua biashara zenu mapema na kufunga usiku, mkiwahudumia wateja kila siku. Mnahakikisha fedha taslimu, salio na chenji vinapatikana, huku jamii ikiendelea kuwaamini,” amesema Favot.
Amesema, kampuni inapanga kuongeza huduma katika vituo vya mawakala ili kupanua vyanzo vyao vya mapato na kuwawezesha kukidhi mahitaji zaidi ya kifedha ya wateja.
Kupitia huduma ya Bustisha Wakala, iliyoanzishwa kwa kushirikiana na Benki ya KCB Tanzania, zaidi ya mawakala 7,000 tayari wanapata msaada wa kuongeza salio la kuendeshea biashara zao kila siku.
Favot aliwahimiza mawakala wengi zaidi kutumia huduma hiyo ili kuimarisha uwezo wao wa kuwahudumia wateja.
Katika mipango yake kuelekea mwaka 2030, Mixx inalenga kuwawezesha mawakala wengi zaidi kutumia zana za kidijitali kusimamia biashara zao na kuwahudumia wateja wengi zaidi.
Aidha, Favot amesema kutakuwa na mikutano ya mara kwa mara kati ya mawakala, yeye mwenyewe na timu ya uongozi wa kampuni.
Mikutano hiyo itawapa mawakala nafasi ya kuwasilisha changamoto, kupendekeza maboresho na kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wao na Mixx.
Favot amewataka mawakala kuendelea kutoa maoni kuhusu uzoefu wao, changamoto wanazokutana nazo katika vituo vyao na huduma zinazohitajika na wateja, ili kusaidia kampuni kuboresha huduma zake.
Kwa upande wake, John Mkwizu, wakala wa Mixx anayefanya shughuli zake eneo la Magomeni, Dar es Salaam, ameeleza umuhimu wa upatikanaji wa salio na matumizi ya zana za kidijitali katika biashara yake.
“Wateja wanatutegemea kupata fedha zao wanapozihitaji. Ninaposhindwa kukamilisha muamala, wanalazimika kutafuta wakala mwingine, nami ninakosa kamisheni.
“Upatikanaji wa salio la uwakala unaniwezesha kuendelea kuwahudumia, huku App ya Mixx Wakala ikinirahisishia usimamizi wa miamala yangu ya kila siku,” amesema Mkwizu.

More Stories
WWF : Ongezeni juhudi katika kuibua masuala ya uhifadhi wa mazingira
Masinga: Mafundi jiungeni na mfumo wa Nest ili kuomba tenda serikalini
Msigwa atoa wito kuandikwa habari za vijijini