November 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WWF : Ongezeni juhudi katika kuibua masuala ya uhifadhi wa mazingira

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

SHIRIKA la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) limewataka waandishi wa habari kuongeza juhudi katika kuandika na kuibua masuala ya uhifadhi wa mazingira, uchumi wa buluu na uwekezaji endelevu ili kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kulinda rasilimali za taifa.

Wito huo umetolewa na Ofisa Programu Mwandamizi wa WWF, Happy Minja, wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari za mazingira yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Mafunzo hayo yaliwakutanisha waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari na kuratibiwa na WWF kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).

Minja amesema uhifadhi wa mazingira ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu katika sekta mbalimbali, hivyo WWF imeamua kuwajengea uwezo waandishi ili watumie nafasi zao kuendeleza ajenda hiyo nchini.

“Sisi kama WWF tunatamani waandishi wa habari waweke mkazo kwenye masuala ya uhifadhi kwa ujumla, kwa sababu uhifadhi na mazingira ni kila kitu. Uhai wetu unategemeana na mazingira,” amesema.

Amesema waandishi wana nafasi kubwa ya kupaza sauti kuhusu changamoto za mazingira na hivyo kusaidia serikali na wadau wengine kuchukua hatua zinazohitajika kulinda mazingira na usalama wa jamii.

Ameongeza kuwa WWF imeamua kufanya kazi na waandishi wa habari kwa kutambua nafasi yao katika kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi, mazingira, uchumi wa buluu na uwekezaji endelevu.

“Tunapowajengea waandishi uwezo, tunaamini watatumia elimu yao kuelimisha taifa na jamii kwa ujumla,” amesema.

Minja amesema mafunzo hayo ni awamu ya nne tangu kuanzishwa kwa programu hiyo mwaka 2022, huku akieleza kuwa yamekuwa yakileta mabadiliko katika uandishi wa habari za uhifadhi na mazingira.

Amesema WWF inajivunia ushirikiano huo kwa kuwa waandishi wamekuwa wakisaidia kuibua changamoto mbalimbali za uhifadhi ambazo zimekuwa zikifanyiwa kazi.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Uhifadhi na Maliasili, Allen Mgaza, amesema ushirikiano unaofanywa na WWF na JET ni muhimu katika kuhakikisha taarifa sahihi kuhusu uhifadhi na mazingira zinawafikia wananchi.

Mgaza amewashauri watekelezaji wa miradi ya maendeleo kuwashirikisha waandishi wa habari tangu hatua za awali za utekelezaji wa miradi hiyo ili kuwawezesha kupata taarifa za kutosha na kuandika habari zenye ufasaha.

“Nadhani kuna haja ya watekelezaji wa miradi kubadilika kwa kushirikisha kundi la wanahabari tangu mwanzo, na si kusubiri hadi kuripoti matokeo au changamoto,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, amesema WWF imekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea uwezo waandishi wa habari wanaoandika masuala ya mazingira na uhifadhi.

Amesema mafunzo hayo yanayofanyika kwa mara ya nne yameongeza uelewa na weledi kwa waandishi ambao wana nafasi muhimu katika kutoa elimu kwa jamii.

“Mafunzo haya ya awamu ya nne yamejikita katika eneo la uchumi wa buluu na uendelevu katika uhifadhi, na tumeona mafanikio makubwa tangu tuanze programu hii,” amesema.

Chikomo amesema JET kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikiwapeleka wanachama wake katika maeneo ya utekelezaji wa shughuli za uhifadhi, ikiwemo mkoani Tanga kujifunza kuhusu nyasi bahari na umuhimu wake katika kulinda mifumo ya ikolojia ya bahari, pamoja na shughuli za wakulima wa mwani.

Amesema awali habari zinazohusu uhifadhi na mazingira hazikuwa zikiandikwa kwa kiwango cha kuridhisha, lakini hali imeendelea kuimarika kutokana na juhudi za kuwajengea uwezo waandishi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Shoroba katika Taasisi ya Kuendeleza Shoroba za Kilimo Tanzania (AGCOT), John Banga, amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha wakulima kutumia mbinu endelevu zinazolinda mazingira.

Banga alisema elimu kwa wakulima kuhusu kilimo endelevu inaweza kusaidia kuboresha uzalishaji na kuhakikisha shughuli za kilimo haziathiri mazingira.

“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha kilimo endelevu kinachotunza mazingira, kutafuta masoko ya kisasa na kufikia azma ya taifa ya uchumi wa buluu na kijani,” amesema.

Ameongeza kuwa kilimo na mazingira vina uhusiano wa karibu kwa kuwa uzalishaji wa kilimo unategemea hali ya hewa, mvua na viumbe mbalimbali wanaochangia kudumisha rutuba na afya ya udongo.