Na Judith Ferdinand,Dodoma
IMEELEZWA kuwa asilimia 65 ya Watanzania wanaishi vijijini huku wakikabiliwa na changamoto ya kutofikiwa na huduma ya vyombo vya habari vingi hapa nchini.
Hivyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa alitoa wito kwa Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania(RUJAT) na waandishi wa habari hapa nchini kuwafikia na kuandika habari za wananchi wa vijijini.

Msigwa amezungumza hayo Oktoba 31,2026 kwenye kongamano la mwaka la tathimini ya huduma za habari na mawasiliano vijijini nchini Tanzania lililoandaliwa na RUJAT,ambapo alisema,kwa sasa takribani asilimia 85 ya vyombo vya habari viko mjini na vinatoa kipaumbele kwa habari za mjini.
Amesema,waandishi wanapaswa kurejea misingi ya uandishi wa habari unaolenga jamii huku akiishauri RUJAT kufanya utafiti wa namna habari za vijijini zinavyopewa kipaumbele na kuanzisha mkakati wa maboresho zaidi.
“Tuongeze kuwa sauti ya wananchi,tuandike habari za watu wa vijijini,mahitaji ya wananchi ya kuelimisha kuhusu maisha yao ni muhimu zaidi.Waandishi tufanye utafiti na uchunguzi,wengi wanazani uchunguzi ni kuhangaika na habari za fulani,”amesema Msigwa.
Sanjari na hayo Msigwa amewataka waandishi wa habari hapa nchini kusimamia taaluma yao na kuinufaisha jamii, badala ya kuacha nafasi hiyo kuchukuliwa na wanaharakati.Ambapo alisema,kuongezeka kwa vyama vingi vya wanaharakati kunachangia wananchi kukosa watetezi wa kweli katika kufikia malengo yao.
“Waandishi simamieni taaluma yenu,kwani wakiwepo wanaharakati wengi kunaleta mgongano katika uandishi. Wakiwepo wanaharakati wa mazingira, uchumi na sekta nyingine, kila mmoja atavutia kwake na kuwaacha wananchi wasio na sauti wakikosa wa kuwasemea,”amesisitiza Msigwa.
Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Meena amesema,mwandishi wa habari anapaswa kuwa sauti ya wananchi badala ya kuwa sauti ya viongozi, akieleza kuwa falsafa hiyo ndiyo msingi wa kuanzishwa kwa chama hicho.
Meena amesema, waandishi wa habari si maadui wa Serikali bali ni wadau wanaoweza kufanya kazi pamoja katika kuhabarisha wananchi hivyo alitoa  wito kwa taasisi za Serikali na wasemaji wake kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari kwa kurahisisha upatikanaji wa taarifa.
“Wakati mwingine waandishi hukutana na vikwazo wanapotafuta ufafanuzi wa masuala ya umma, hivyo ni muhimu watendaji kuelewa majukumu yao na kutoa taarifa kwa wakati,”amesema Meena.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa RUJAT, Prosper Kwigize amesema,chama hicho kilianzishwa mwaka 2020 likiwa na waandishi 20 waliokutana Dodoma baada ya kujifunza mifumo ya uandishi wa habari za vijijini katika nchi nyingine na kubaini umuhimu wa Tanzania kuwa na taasisi maalumu inayosimamia eneo hilo.

Kwigize amesema,waandishi wa habari wanapaswa kuachana na uandishi unaotegemea mikutano na taarifa kwa vyombo vya habari na badala yake kwenda kwa wananchi kutafuta habari zenye matokeo.
Amesema,moja ya malengo makuu ya chama hicho ni kuondoa mtazamo unaoyapa kipaumbele zaidi maeneo ya mijini katika kuripoti habari huku akisitiza kuwa habari za vijijini zina thamani sawa na za mijini kwa sababu maendeleo ya maeneo hayo yanategemeana.Â
Naye Mbunge wa Jimbo la Bunda Esther Bulaya,ametoa ushauri kwa chama hicho pamoja na waandishi wa habari kwa ujumla kurejesha ubora wa uandishi uliokuwepo zamani,ambapo alisisitiza kuwa ushindani wa kitaaluma, bidii, ubunifu na uchunguzi ndivyo vilivyojenga waandishi mahiri huku akisisitiza kuwa mwandishi hapaswi kuishia kuripoti matukio ya kawaida bali kuwa na uwezo wa kuona masuala yanayohitaji kuchunguzwa na kuandikwa kwa kina.Â




More Stories
Masinga: Mafundi jiungeni na mfumo wa Nest ili kuomba tenda serikalini
Exim Tanzania yaunga mkono uhifadhi wa Mazingira,Maendeleo
TCB kugawa pembejeo kidijitali