October 31, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Tulia atoa vifaa kukamilisha ujenzi daraja Itezi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya

SPIKA Mstaafu wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson, ametoa msaada wa vifaa vya ujenzi, vikiwemo saruji, kokoto, nondo na mchanga, kwa wananchi wa Mtaa wa Itezi Mashariki, Kata ya Nsalaga jijini Mbeya, ili kuwawezesha kukamilisha ujenzi wa daraja litakalosaidia kutatua changamoto ya usafiri inayowakabili wakazi wa eneo hilo.

Dkt. Tulia ametoa msaada huo baada ya kuguswa na juhudi za wananchi walioamua kuchangishana fedha na kuanza ujenzi wa daraja hilo kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya kuvuka eneo hilo, hasa wakati wa mvua, hali ambayo imekuwa ikiathiri shughuli za kiuchumi na kusababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo yaliyofanyika Oktoba 30, 2026, mwakilishi wa Mbunge huyo, Stephen Chambanenge, amesema Dkt. Tulia alipata taarifa za changamoto hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Itezi Mashariki, aliyemweleza kuhusu hatua zilizokuwa zimeanza kuchukuliwa na wananchi kutafuta suluhisho.

Amesema juhudi za wananchi hao zimeonesha dhamira yao ya kutatua changamoto zinazowakabili, hivyo ofisi ya Mbunge imeamua kuungana nao kwa kutoa msaada huo, huku akieleza matarajio ya kupata ushirikiano zaidi kutoka serikalini.

“Wananchi walishachukua hatua ili kujinusuru na changamoto ya El Niño na kukabiliana na tatizo hilo. Mngeweza kusubiri Serikali ije, lakini ninyi mmeanza kwanza kuonyesha nguvu zenu. Sasa wadau wamejitokeza, ikiwemo ofisi ya Mbunge, kuwaunga mkono. Tunatarajia Serikali nayo itawaunga mkono katika kukabiliana na mvua za El Niño,” amesema Chambanenge.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Itezi Mashariki, Lameck Daudi, amesema eneo hilo limekuwa likikumbwa na mafuriko yanayotokana na maji mengi yanayotiririka kutoka Bonde la Uyole, hali inayosababisha athari mbalimbali kwa wakazi.

Amesema pamoja na daraja linalojengwa sasa, wananchi wana mpango wa kujenga madaraja mengine katika maeneo yenye changamoto, ikiwemo Mto Nsalaga na eneo lililo chini ya reli.

“Hapa tunajenga daraja dogo la kupitisha maji. Mashariki mwa eneo hili tuna Mto mkubwa wa Nsalaga ambako nako tutajenga madaraja makubwa. Ujenzi tayari umeanza, kinachobaki ni kufunika. Pia tuna kivuko kingine chini ya reli ambacho tunatarajia kuanza kukijenga, hivyo tunaendelea kutafuta fedha,” amesema Daudi.

Naye Diwani wa Kata ya Nsalaga, Clemence Mwandemba, amesema kata hiyo ipo katika mazingira hatarishi kutokana na jiografia yake ya kuwa bondeni, huku maji yanayotiririka kutoka maeneo mbalimbali, yakiwemo yanayopitishwa kupitia makalavati makubwa ya mradi wa barabara ya Njia Nne, yakielekezwa katika kata hiyo.

Amesema bado kuna uhitaji mkubwa wa msaada kutoka ofisi ya Mbunge ili kukabiliana na changamoto hiyo, akieleza kuwa wananchi wamekuwa wakijitolea kujenga madaraja katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi na wakazi wengine wanapata njia salama za kupita.

Naye mkazi wa Mtaa wa Itezi Mashariki, Yohana Msafiri, amesema kukosekana kwa daraja salama kumekuwa kukiwapa wakati mgumu wakazi wa eneo hilo, hususan watoto wanaokwenda shule na wazee, huku baadhi ya wananchi wakipata majeraha wanapojaribu kuvuka.

Amesema msaada uliotolewa na Dkt. Tulia umewapa matumaini ya kukamilisha ujenzi wa daraja hilo na kupata suluhisho la changamoto hiyo, hasa wanapoelekea katika kipindi cha mvua kubwa.